Carol Muthoni afichua kuwa Mulamwah alimpata akiwa kwenye mahusiano mengine

Muhtasari

•Muthoni alisema hawakuchumbiana na Mulamwah mara moja kwa kuwa wakati huo alikuwa kwenye mahusiano magumu.

•Muthoni alisema alikuwa na matumaini makubwa kuhusiana na mahusiano yao na ndoto yake ilikuwa kuzeeka pamoja na mchekeshaji huyo. 

Image: INSTAGRAM/CAROL SONNIE

Mwigizaji Caroline Muthoni almaarufu Carrol Sonnie amefichua kuwa tayari alikuwa kwenye mahusiano mengine wakati walipopata na mchekeshaji Mulamwah kwa mara ya kwanza.

Akiwa kwenye mahojiano na Dr Ofweneke, Muthoni alisema walikutana na baba ya binti yake mwaka wa 2017 katika majaribio ya uigizaji yaliyofanyika Kenya National Theatre.

Muthoni alisema hawakuchumbiana na Mulamwah mara moja kwa kuwa wakati huo alikuwa kwenye mahusiano magumu.

"Alikuwa ananikatia nikamwambia siwezi chumbiana naye kwa wakati huo kwa kuwa niko kwenye mahusiano magumu. Nilikuwa napanga kukatiza uhusiano wangu na mpenzi wangu wa wakati huo. Mulamwah alikuwa ananisumbua sumbua alafu mwaka wa 2018 tukaanza kuchumbiana," Muthoni alisema.

Mama huyo wa mtoto mmoja alisema ilimchukua miezi mitatu pekee baada ya kuachana na mpenzi wake kujitosa kwenye mahusiano na Mulamwah.

"Tulikuwa tunapatana mara kwa mara na nikaanza kumpenda. Nilipenda utu wake. Yeye ni mtu mzuri, anaelewa  na alikuwa ananisaidia sana. Alinisaidia kutengeneza chapa yangu," Alisema.

Muthoni alisema alikuwa na matumaini makubwa kuhusiana na mahusiano yao na ndoto yake ilikuwa kuzeeka pamoja na mchekeshaji huyo. 

"Nilitaka tuwe na mustakabali pamoja. Sipezi chochote kumhusu, nilisahau sasa. Kitu nimekubali kuachilia hakuna haja ya kupeza," Alisema.

Muthoni hata hivyo  alikiri kuwa alichangia katika kuvunjika kwa mahusiano yao ya miaka minne mwaka uliopita.