Diamond amshukuru Zuchu kwa zawadi ya nguo kali

Muhtasari

• Msanii Diamond Platnumz wikendi iliyopita alidhihirisha wazi kwamba nguo alikuwa amevalia alipewa na msanii mwenza Zuchu.

• Alimshukuru Zuchu kwa nguo hiyo.

Diamond Platnumz
Image: INSTAGRAM

Wikendi iliyopita staa wa Bongo Fleva Diamond Platnumz alikuwa katika ziara inayotajwa kuwa ya kimuziki nchini Nigeria ambapo alikuwa amevalia nguo moja matata maelezo hamna.

Wengi walifurahishwa na nguo hiyo ambayo walimsifia kwa muonekano mzuri ambao ni kawaida yake ila safari hii jamaa kaenda mno na alipakia kwenye instastories zake akitoa shukrani kwa mtu aliyempa ile nguo kali.

“Thanks Zuchu for the fit.” Aliandika Diamond kwenye instastories zake ambapo wengi waliipata siri yenyewe kwamba kupembeza kwake kulichangiwa pakubwa na msanii mwenza kutoka lebo yake ya WCB Wasafi, Zuchu.

Wawili hao wamekuwa wakisemekana kuwa na mahusiano ya kichini chini ya mapenzi ambapo Zuchu ameonekana akijikwaa ulimi katika mahojiano kadha ambayo amefanya na pindi swali hilo linapoulizwa yeye hugeuka kigugumizi ghafla.

Mwezi jana palikuwa na uvumi wa wawili hao kufanya ndoa sambamba na siku ya wapendanao ya Valentino, jambo lililokuja baadae kugeuka kuwa ni kiki walikuwa wakifukuzia mitandaoni ili kuvutia umati kwa tamasha kubwa waliloliandaa kwa jina la ‘Mahaba ndi ndi ndi’

Wawaili hao kila mmoja alijitokeza wazi na kusema kwamba hayupo single na kwamba yupo katika mahusiano lakini si Diamond wala Zuchu aliyeweka wazi kuhusu jina au muonekano wa mpenzi wake, jambo lililozidisha uvumi kwamba huenda wanapendana na kila mmoja akitaja kuwa katika mahusiano maanake walikuwa wanazungumzia mahusiano yayo hayo mamoja kwa lugha fiche.

Diamond anatazamia kuachia EP yake ya kwanza kabisa kwa jina la First of All mnamo Machi 11, EP ambayo imesubiriwa kwa raghba ya mkanja haswa ikizingatiwa ndio yake ya kwanza tangu aingie kwenye muziki.

Je, unahisi bado Diamond na Zuchu ni kiki wanafukuzia mitandaoni ama wapo kwenye mapenzi ya siri?