Ninajuta kusema ndoa ni ulaghai - DJ Crème baada ya kuungana tena na mkewe

Muhtasari
  • Katika mahojiano, DJ Crème alikiri kwamba anajuta kulaani ndoa na kumfanya mkewe kukosolewa na kukaguliwa na umma

Mcheza santuri maarufu George Njuguna, almaarufu DJ Crème de la Crème, amethibitisha kuungana na kurejesha mapenzi yake na mkewe na mama ya watoto wao wawili, Denise 'Dee'.

Katika mahojiano, DJ Crème alikiri kwamba anajuta kulaani ndoa na kumfanya mkewe kukosolewa na kukaguliwa na umma.

“Baada ya muda niligundua kuwa nimefanya kosa kubwa, hasa kusema Ndoa ni utapeli. Hizo zilikuwa ni hisia tu na ninajuta sana kwa sababu zimenigharimu vitu vingi. Je, unaweza kufikiria watoto wangu katika siku zijazo watakuja kunionyesha video ya YouTube wakisema Baba kwa nini ulisema ndoa ni ulaghai?

Kauli nzima ilitokana na mihemko na hakuna kitu kikubwa, lakini unagundua kuwa mke wako lazima arudi nyumbani na nikagundua pia nyumba ilikuwa tupu bila yeye," alikiri DJ Crème De La Crème.

Alisema kuwa anafurahi kuona familia yake ikirudi pamoja, hisia anazosema ni ngumu kuelezea.

"Familia inaendelea vizuri, wamerudi nyumbani na wametulia sasa. Mungu ni mwenye neema ya kutosha alirudisha familia na inashangaza,Siwezi hata kuelezea hisia

Ndio ndio hata yuko Jikoni anatengeneza chakula na hata naona nikiacha kukonda nilikuwa nimekonda,” Crème Alisema.

Hata hivyo, DJ huyo alichagua kutotoa maelezo kuhusu jinsi walivyofaulu kukarabati ndoa yao, akikiri kuwa kila ndoa ina misukosuko yake.