Hadithi ya mvulana aliyeangamiza familia yake kuangaziwa katika filamu

Muhtasari

• Hadithi hiyo ambayo si ya kurubuni bali ya kuzungumzia matukio halisi jinsi yalivyotokea itaangaziwa katika sehemu ya nne ya msimu wa pili wa muendelezo wa filamu hiyo ya uchunguzi.

Mshukiwa Lawrence Warunge
Mshukiwa Lawrence Warunge

Kumekuwa ni minong’ono mitandaoni baada ya baadhi ya watu na wapenzi wa filamu nchini Kenya kusambaza uvumi kwamba hadithi ya kweli ya mvulana aliyeangamiza familia yake yote inatarajiwa kupeperushwa kama filamu.

Katika taarifa iliyoonekana kwenye baadhi ya blogu za humu nchini, hadithi ya Lawrence Waruinge itapeperushwa kama filamu maarufu ya Crime and Justice katika kipindi kiitwacho "Slaughter House" kitakachopatikana kwenye Showmax.

Hadithi hiyo ambayo si ya kurubuni bali ya kuzungumzia matukio halisi jinsi yalivyotokea itaangaziwa katika sehemu ya nne ya msimu wa pili wa muendelezo wa filamu hiyo ya uchunguzi inayojumuisha mwigizaji wa zamani wa Zora, Sarah Hassan na mwigizaji Alfred Munyua wanaoigiza kama makachero Makena na Silas mtawalia.

Mnamo Januari 2021, mwanafunzi wa chuo kikuu Lawrence Warunge alidaiwa kuwaua watu wanne wa familia yake na mfanyikazi wa shambani nyumbani kwao Kiambu.

Baadaye alifichua kwamba alihamasishwa na Villanelle, muuaji asiye na kigugumizi wa Jodie Comer katika filamu yenye ukakasi wa kijasusi ya Uingereza, Killing Eve.

 Kulingana na fununu hizo, inadaiwa tukio hilo la kusikitisha, ambalo lilitikisa taifa na kusambaa kwa wiki kadhaa, lilihimiza kipindi  hicho cha ‘Slaughterhouse’ katika tamthilia ya Crime and Justice.

Warunge alikamatwa na maafisa wa polisi mnamo Januari 9, 2021, baada ya maafisa wa polisi kumnasa kutoka mafichoni huko Kabete, Kaunti ya Kiambu. Alishtakiwa kwa kumuua babake, mamake, kakake na mkulima nyumbani kwao Kiambu.

 Waruge mwenye umri wa miaka 22 hapo awali alikiri kutekeleza mauaji mengi alipohojiwa na DCI. Madai yake yalithibitishwa na ripoti za uchunguzi wa maiti ya marehemu wa familia yake. 

Mpenzi wake Sarah Muthoni, ambaye alitajwa kama mwandani wake pia aliwekwa chini ya ulinzi wa polisi. Kulingana na maafisa hao wa upelelezi, Warunge alikuwa amemshawishi Muthoni kumsaidia, huku akimuahidi maisha bora na ya amani pindi watakapolimaliza Sakata hilo. 

Hata hivyo, upande wa mashtaka ulimgeuza Muthoni kuwa shahidi wa serikali kusaidia katika kumchunguza mpenzi wake. Wawili hao walifanyiwa uchunguzi wa kiakili ambao ulitangaza kuwa hawakufaa kupandishwa kizimbani kujibu mashtaka dhidi yao.