Mwanaume ashtakiwa kwa kumhadaa mwanasiasa kwa picha za uchi

Muhtasari

• Mwanaume mmoja alifikishwa katika mahakama ya Milmani jijini Nairobi kwa tuhuma ya kumrubuni pesa mgombea wa uwakilishi wa kike Vihiga.

• Mwanaume huyo alimtumia mwanasiasa huyo picha zake za uchi kupitia WhatsApp na kumshrutisha amlipe la sivyo angezivujisha picha hizo.

Image: jackline Mwenesi (Facebook)

Mwanaume mmoja alifikishwa katika mahakama ya Milmani jijini Nairobi kwa tuhuma ya kumrubuni pesa mgombea wa uwakilishi wa kike Vihiga kwa kile kilitajwa kama ni kumtishia mwanasiasa huyo kuvujisha picha zake za uchi.

Mwanasiasa huyo kwa jina Jackline Mwenesi ambaye analenga kuwakilisha kina mama bungeni kwa tiketi ya chama cha UDA aliiambia mahakama kwamba mwanaume huyo kwa jina Tyson Wabuti alimtumia picha hizo zake za soni kupitia WhatsApp na akamtaka amtumie pesa la sivyo angezivujisha na kumchafulia jina kwa wapiga kura na wafuasi wake.

Mwenesi kwa kuhofia kuchafuliwa jina, alimtumia Wabuti shilingi elfu 5 mwanzo na kisha baadae akampa elfu 37, jumla ya elfu 42 za Kenya ili kulinda haiba kubwa ya jina lake.

Baadae alipiga ripoti katika kituo kimoja cha polisi jijini Nairobi kulingana na taarifa katika kituo kimoja cha runinga humu nchini.

Baadae mshukiwa huyo alitiwa nguvuni baada ya udadisi wa kijasusi kutoka makachero wa DCI na kufikishwa mahakamani ambapo alipatikana na simu tatu za kufanya utapeli mitandaoni.

Mshukiwa huyo aliyekamatwa Ijumaa wiki jana alilazimika kushikiliwa kwa siku nyingine zaidi ili kutoa nafasi kwa uchunguzi wa kina kukamilika kabla ya kufunguliwa mashtaka ya utapeli wa mitandaoni.