"Sijawahi zaa nje ya ndoa!" KRG the Don asema

Muhtasari

• Kuna mtu anasema eti niko na binti mahali ambaye alizaliwa mwaka 2002, tafadhali jaribu michezo hiyo yenu ya kipumbavu mahali kwingine.

KRG the Don
KRG the Don
Image: maktaba

Msanii wa dancehall KRG the Don ameweka wazi kuhusu uvumi unaotembezwa mitandaoni kwamba aliwahi zaa mtoto wa kike ambaye kwa sasa amemtelekeza.

Msanii huyo ambaye mwishoni mwa mwaka jana alitangaza kutalikiana na mkewe halali alijipata katika mtanange huo baada ya shabiki mmoja kumuandikia kwamba aache kujionesha na maisha ghali mitandaoni ilhali mwanawe anateseka katika mitaa ya mabanda.

KRG alimjibu kwa kusema kwamba hajawahi zaa mtoto nje ya ndoa na kwamba watoto pekee ambao amezaa ni wanne tena wote wa kiume na mpaka akaenda mbele kuwataja kwa majina huku akipuuzilia mbali madai ya kuwa na binti.

Alipinga madai hayo kwamba mtoto huyo anayesemekana ni wake na ambaye alizaliwa mwaka 2002 si wake kwa sababu haiwezekani kipindi hicho alikuwa bado hajabaleghe.

“Watu wangu kuna uvumi nimekuwa nikisikia kwa wiki kadhaa zilizopita lakini sasa wacha niweke kila kitu paruwanja kabla wakuza maudhui hawajaponyoka na madai hayo. Kuna mtu anasema eti niko na binti mahali ambaye alizaliwa mwaka 2002, tafadhali jaribu michezo hiyo yenu ya kipumbavu mahali kwingine kwa sababu mimi mwaka huo nilikuwa na miaka 11 pekee na haileti uhalisia hata kidogo kusema kwamba ningeweza kutia mimba. Nina watoto wanne tu, na wote ni wa kiume,” alisema KRG the Don.