"Tutawasurprise na harusi" Akuku Danger adokeza kuhusu ndoa, kupata mtoto na Sandra Dacha

Akuku alifichua kwamba amekuwa akichumbiana na Dacha kwa kipindi cha miezi sita.

Muhtasari

•Akuku alidokeza kwamba anapanga kufunga pingu za maisha na mwigizaji huyo wa Auntie Boss hivi karibuni.

Image: INSTAGRAM// AKUKU DANGER

Mchekeshaji wa Churchill Show Mannerson Oduor almaarufu Akuku Danger amesisitiza kwamba ana mahusiano ya kimapenzi na mwigizaji Sandra Dacha.

Akizungumza kwenye tamasha ya 'One Mic' ambayo ililenga kuchangisha bili yake ya hospitali, Akuku alidokeza kwamba anapanga kufunga pingu za maisha na mwigizaji huyo wa Auntie Boss hivi karibuni.

"Sandra ni mpenzi wangu. Hivi karibuni tutawashangaza muone harusi ndio watu waanze kuamini. Ama mtaona mimba ndio muamini. Yeye ni mpenzi wangu," Akuku alisema.

Mchekeshaji huyo ambaye alipigania maisha yake hospitalini kati ya mwezi Desemba na Januari alifichua kwamba amekuwa akichumbiana na Dacha kwa kipindi cha miezi sita.

"Tumekuwepo hapa na pale. Tuko na raha," Alisema

Dacha ni mmoja wa watu ambao walisimama na mchekeshaji huyo zaidi katika kipindi ambacho alikuwa anaugua.

Alienda hospitalini mara kwa mara kumuona mpenzi huyo wake na kuhamasisha watu kuchangia bili yake ya hospitali.