Will Smith amzaba kofi ya usoni mchekeshaji Chris Rock jukwaani kwa kumkejeli mkewe

Muhtasari

•Will Smith amemzaba kofi Chris Rock jukwaani wakati wa utoaji wa Tuzo za Oscars baada ya mchekeshaji huyo kufanya mzaha kuhusu mke wa mwigizaji huyo, Jada Pinkett Smith.

• Smith alipokuwa anarudi kukaa kwenye kiti chake alimkemea Rock  "kutolitaja jina la mke wangu,"

Will Smith akimzaba kofi Chris Rock
Will Smith akimzaba kofi Chris Rock
Image: BBC

Will Smith amemzaba kibao cha usoni Chris Rock jukwaani wakati wa utoaji wa Tuzo za Oscars baada ya mchekeshaji huyo kufanya mzaha kuhusu mke wa mwigizaji huyo, Jada Pinkett Smith.

Akizungumzia mtindo wa nywele za Pinkett Smith, Rock alisema: "Jada, anasubiri kwa hamu GI Jane 2."

Jada aliwahi kuzungumzia huko nyuma kuhusu matatizo yake ua nywele.

Alisema: "Nimekuwa na matatizo ya kupoteza nywele. Wakati inaanza (hali hii) ilikuwa ya kutisha." Jada aliongeza "Ilikuwa moja ya nyakati hizo katika maisha yangu ambapo nilikuwa nikitetemeka kwa hofu," alielezea. "Ndio sababu nilikata nywele zangu na naendelea kuzikata."

Katika tukio la usiku wa Oscers Smith alipanda jukwaa na kumshambulia Rock kabla ya kurudi kwenye kiti chake akiongea kwa sauti: "acha kutaja jina la mke wangu."

Smith baadaye aliomba msamaha katika hotuba yake ya kupokea tuzo mwigizaji bora. Tuzo za Oscars zinatajwa kama tuzo kubwa zaidi za masuala a filamu duniani.

"Naomba radhi kwa wandaaji wa tuzo, naomba radhi kwa wasanii wenzangu wote tunaowania tuzo," Smith alisema baada ya kushinda tuzo ya kwanza ya Oscar katika maisha yake ya Sanaa kupitia kazi yake aliyocheza kama baba kwenye filamu ya maisha ya wakali wa Venus na Serena William.

"Sanaa inaiga maisha. Ninaonekana kama baba mwendawazimu, kama vile walivyosema kuhusu Richard Williams. Lakini upendo utakufanya ufanye mambo ya ajabu."

Wenzi hao walikuwa wakitabasamu mapema jioni kwenye zulia jekundu
Wenzi hao walikuwa wakitabasamu mapema jioni kwenye zulia jekundu
Image: BBC

Rock alionekana kushtushwa baada ya tukio hilo, akiwaambia wasikilizaji: "Huo ulikuwa usiku mkubwa zaidi katika historia ya matukio ya televisheni."

Kisha akakabidhi tuzo bora ya Makala bora, ambayo ndiyo sababu aliyompeleka jukwaani.

Utani wake kuhusu Jada na nywele zake ulikuwa ukirejea filamu ya mwaka 1997, GI Jane, ambayo Demi Moore alicheza nafasi ya mtu mwenye nywele fupi sana (karibu na kipara).

Mshtuko wa nyuma ya Jukwaa

Image: BBC

Nyuma ya jukwaa 'Backstage' katika ukumbi wa michezo wa Dolby huko Los Angeles, waandishi walipatwa na mshtuko kuhusu tukio hilo.

Waandishi wa habari walikuwa wakishiriki katika mkutano na waandishi wa habari ambapo washindi walikuwa wakienda baada ya kutoa hotuba zao za kupokea tuzo.

Lakini ghafla macho na masikio yalikuwa kwenye skrini kuangalia kile kilichokuwa kikiendelea kwenye utoaji wa tuzo jukwaani, ilionekana wazi kuna jambo kubwa linatokea.

Mara ya kwanza, ilionekana kama utani au kitu kilichopangwa. Smith hata alionekana awali kucheka baada ya Rock kutoa utani wake juu ya mke wake akionekana kama G.I. Jane.

Jada alionekana kukasirika, lakini kwa wakati huu ilidhaniwa kuwa hii ilikuwa sehemu ya aina fulani ya utani uliopangwa kabla.

Shaka ilianza pale Smith alipoinuka kutoka kwenye kiti chake na kwenda jukwaani kumzaba kofi Rock.

Hakuna shaka yoyote kwamba, hawa wote wawili ni wakongwe wa filamu na televisheni, na wana uwezo mkubwa wa kutengeneza tukio la 'kofi bandia'.

Lakini wakati Smith anarudi kukaa katika kiti chake na kupiga kelele kwa Rock "kutolitaja jina la mke wangu," ilikuwa wazi kwamba tukio hili sio la kuchorwa au kupangwa.

Watazamaji nyumbani hawakuweza kusikia mengi. Kwa sababu Mtandao wa matangazo wa ABC ulikuwa umekata matangazo ya moja kwa moja kuepuka kuwakwanza watazamaji walioko nyumbani.

Kulikuwa na ukimya katika chumba walichokuwa washindi wa tuzo hizo. Wafanyakazi wa tuzo walionekana kushtushwa kama ilivyo kwa waandishi wa habari. "Nilidhani walikuwa wanafanya mzaha kidogo," mmoja alimwambia mwenzake.

Rock, wakati huo huo, ulionekana kutikiswa. Lakini, akitambua kuwa alikuwa ameweka historia katika tuzo za Oscars, alijaribu kupoza hali ya mambo kwa kusema: "Huo ulikuwa usiku mkubwa zaidi katika historia ya televisheni."

Katika hotuba yake muda mfupi baada ya tukio la kumchapa kofi Rock, alihitimisha kwa kusema "natumai waandaji wa tuzo watanialika tena'.

Kwa mujibu wa Scott Feinberg wa Hollywood, baada ya tukio hilo na wakati wa mapumziko ya tangazo, Smith aliyekuwa anabubujikwa na machozi alihitaji "kuwekwa kando na kufarijiwa" na Denzel Washington na Tyler Perry.

"Will na Chris, tutatatua tatizo hili kama familia. Hivi sasa tunaendelea na upendo," alisema Sean "Diddy" Combs, aliyekuwa akiwasilisha kipengelea kilichofuata kwenye tuzo hiyo.

Mbali na Smith, washindi wengine katika tuzo hizo za Jumapili usiku ni pamoja na Jessica Chastain, ambaye alichukua tuzo ya mwigizaji bora kupitia The Eyes of Tammy Faye; Jane Campion, ambaye alishinda tuzo ya muongozaji bora kupitia The Power of the Dog; huku Apple TV film Coda ikishinda kama filamu bora

Katika tuzo hizo za 94, tuzo ya mugigaji bora msaidizi wa kike imeenda kwa Ariana DeBose kupitia West Side Story, Troy Kotsur akishinda muigizaji bora msaidizi wa kiume kupitia Coda, huku tuzo sita zikienda Dune.