'Huenda nikawa mjamzito tena mwaka huu' Vera afunguka tamaa yake ya kupata mtoto mwingine na Mauzo

Muhtasari

•Vera amefichua kwamba hivi majuzi yeye na mumewe Brown Mauzo wamekuwa na tamaa kubwa ya kupata mtoto wao wa pili.

•Vera amefichua kwamba mahusiano yake na Mauzo ndiyo marefu zaidi kuwahi kuwa nayo katika maisha yote akiwa  mtu mzima.

Image: INSTAGRAM// VERA SIDIKA

Takriban miezi mitano tu baada ya kujifungua mtoto wake wa kwanza, mwanasoshalaiti Vera Sidika amedokeza kwamba huenda tukamuona amebeba ujauzito mwingine hivi karibuni.

Mama huyo wa binti mmoja amefichua kwamba hivi majuzi yeye na mumewe Brown Mauzo wamekuwa na tamaa kubwa ya kupata mtoto wao wa pili. Mara hii, wawili hao wanatamani kupata mtoto wa kiume.

"Nina tamaa kubwa ya mtoto. Kweli, sio mimi tu, mume wangi  pia. Tunataka mtoto mwingine. Kwa matumaini, mvulana. Labda tunapaswa kuzingatia hilo  na kujaribu. Kwa kiwango hiki, Mtu huenda akawa mjamzito tena mwaka huu," Vera aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Mwanasoshalaiti huyo mwenye umri wa miaka 32 amedai anatazamia sana kukuza familia yake na Mauzo.

"Mume wangu na Asia ni baraka. Ninaishi maisha ya ndoto yangu. Mungu ailinde familia yetu," Alisema.

Vera amefichua kwamba mahusiano yake na Mauzo ndiyo marefu zaidi kuwahi kuwa nayo katika maisha yote akiwa  mtu mzima.