"Haikupaswa kuwa hivi karibuni!" Mpenzi wa Baha wa Machachari akiri hawakupangia mimba yake

Muhtasari

•Georgina aliweka wazi kwamba yeye na mpenzi wake waliwahi kuzungumzia suala la kupata watoto ila hawakukusudia kutimiza mpango huo hivi karibuni.

•Malkia huyo mwenye umri wa miaka 21 pia alifichua  hawajakuwa wakitumia mbinu zozote za kupanga uzazi.

Image: INSTAGRAM// GEORGINA NJENGA

Mpenzi wa mwigizaji Tyler Kamau Mbaya almaarufu Baha, Bi Georgina Njenga amefichua kwamba ujauzito wake wa sasa sio jambo ambalo walipangia.

Akishirikisha wafuasi wake wa Instagram katika kipindi cha maswali na majibu, Georgina aliweka wazi kwamba yeye na mpenzi wake waliwahi kuzungumzia suala la kupata watoto ila hawakukusudia kutimiza mpango huo hivi karibuni.

"Tumekuwa tukiishi pamoja kwa kipindi cha miaka miwili sasa, kwa hivyo tulikuwa tumezungumzia suala la kupata watoto, lakini haikupaswa kuwa hivi karibuni. Hata hivyo, pia tulikuwa tumekubaliana kuwa ikitokea tutakuwa sawa kupata mmoja," Georgina alimjibu shabiki aliyetaka kujua ikiwa walikuwa wamepanga kupata mtoto.

Malkia huyo mwenye umri wa miaka 21 pia alifichua  hawajakuwa wakitumia mbinu zozote za kupanga uzazi.

Alisema amekuwa akibeba ujauzito wake wa sasa kwa zaidi ya miezi mitano. Hata hivyo watu wengi wakiwemo marafiki na baadhi ya wanafamilia walikuja kujua kuhusu hali yake hivi majuzi walipotangaza kwenye mitandao ya kijamii.

"Marafiki wengi wetu walijua jana (Jumatatu). Tuliambia wanafamilia wa karibu," Georgina alimjibu shabiki aliyetaka kujua jinsi marafiki wao na familia ilichukulia habari kuhusu ujauzito wake.

Georgina na Baha walitangaza kuhusu ujauzito wa mtoto wao wa kwanza siku ya Jumatatu kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii.