"Naomba apate raha, upendo na amani" Briana afichua sababu za kutengana na Harmonize

Muhtasari

•Malkia huyo ambaye amekuwa na Harmonize kwa chini ya mwaka mmoja aliweka wazi kuwa kwa sasa yupo nyumbani kwao Australia.

Harmonize na Briana
Harmonize na Briana
Image: INSTAGRAM// HARMONIZE

Mlimbwende kutoka Austrialia, Briana Jai amethibitisha kwamba hayupo tena kwenye mahusiano na staa wa Bongo, Harmonize.

Akizungumza kupitia kanda ya video ambayo alipakia Instagram, Briana alifichua kwamba imekuwa muda sasa tangu mahusiano yao yalipogonga ukuta.

Briana ambaye alikuja kujulika kama mpenzi wa Harmonize mwezi Novemba, mwaka jana amesema vipaumbele vyao maishani vilikosa kuwiana na ndiposa wakaafikiana kutengana.

"Mahusiano yetu hatimaye yalikosa kufanikiwa.Nilihisi vipaumbele vya kile tulichotaka na maisha yetu vilikuwa tofauti. Hata hivyo tulikuwa na miezi michache mizuri pamoja. Sitasahau kamwe kumbukumbu tulizoshiriki pamoja na naomba apate raha, upendo na amani. Napeza familia yangu ya Tanzania, nawapenda sana," Briana alisema.

Malkia huyo ambaye amekuwa na Harmonize kwa chini ya mwaka mmoja aliweka wazi kuwa kwa sasa yupo nyumbani kwao Australia.

Ingawa mahusiano yake na Harmonize yalikosa kufua dafu, Briana ameahidi kuzuru Tanzania katika siku za usoni.