Rev Victor Githu azungumzia madai kwamba alipata alama 227 katika KCPE

Muhtasari

•Githu ambaye ana umri wa miaka 12 amesema huo ni uvumi usio na msingi huku akibainisha wazi kuwa bado yupo katika darasa la sita.

•Vilevile alilaani ripoti zilizodai kwamba alijaribu kujitoa uhai asubuhi ya Jumanne kutokana na msongo wa mawazo uliomkumba baada ya kupokea matokeo ya KCPE.

Image: FACEBOOOK//VICTOR GITHU

Mhubiri mdogo zaidi kuwahi pata umaarufu mkubwa nchini Kenya, Victor Githu amepuuzilia mbali madai kuwa alijizolea alama 227 katika mtihani wa KCPE 2021.

Githu ambaye ana umri wa miaka 12 amesema huo ni uvumi usio na msingi huku akibainisha wazi kuwa bado yupo katika darasa la sita.

"Mimi najiuliza ilitokea lini nikawa mtahiniwa. Nilifanya KCPE vipi? Sijafanya KCPE! Huo ni uvumi tu. Wanasema nilipata 227, hata kama ningefanya mtihani huo najua Mungu angenipendelea. Najua nimebarikiwa na hekima, ningefanya vizuri kuliko hiyo," Victor alisema akiwa kwenye mahojiano na Eve Mungai.

Mchungaji huyo mdogo jasiri amewakosoa wale ambao wamekuwa wakieneza uvumi hasi kumhusu. Hata hivyo aliweka wazi kuwa hajalishwi na maoni ya watu.

Victor alifichua kwamba yeye ni mwanafunzi shupavu na mara nyingi huibuka miongoni mwa wanafunzi bora shuleni.

"Kama ningekalia mtihani huo labda hata ni mimi ningeibuka bora. Ningekuwa mwanafunzi anayeongoza," Alisema.

Victor amewaomba wanaofuatilia maisha yake wasubiri wakati wake wa kufanya mtihani huo ufike huku akiahidi kuweka matokeo yake wazi atakapoyapokea.

Vilevile alilaani ripoti zilizodai kwamba alijaribu kujitoa uhai asubuhi ya Jumanne kutokana na msongo wa mawazo uliomkumba baada ya kupokea matokeo ya KCPE.

"Mimi nilichokunywa asubuhi nimaji na chai pekee kisha nikaenda shule. Sijui wanachozungumzia. Labda tu niwe nimeshambuliwa na mazingaombwe, mimi niko na Mungu," Victor alisema.