Simon Kabu akiri kuwa na binti wa miaka 24 nje ya ndoa, azungumzia tetesi za kuvunjika kwa ndoa yake

Muhtasari

•Kabu alisisitiza kwamba bado yupo kwenye ndoa na mke wake anayejulikana, Sarah Kabu na kupuuzilia mbali  madai ya kuwa na mpango wa kando.

•Kabu hata hivyo alikiri kuwa na binti mkubwa mwenye umri wa miaka 24 ambaye alipata kabla ya kufunga ndoa na Sarah.

Simon Kabu na mkewe Sarah Kabu
Simon Kabu na mkewe Sarah Kabu
Image: HISANI

Huku kukiwa na wasiwasi kuhusu hali ya sasa ya ndoa yake, mwanzilishi wa Bonfire Adventures Simon Kabu alishirikisha wafuasi wake kwenye kipindi cha maswali na majibu. (Q&A)

Maswali mengi ambayo yalielekezwa kwa bosi huyo wa kampuni kubwa ya kusafirisha watalii ni kuhusu ndoa na mahusiano yake.

Kabu alisisitiza kwamba bado yupo kwenye ndoa na mke wake anayejulikana, Sarah Kabu na kupuuzilia mbali  madai ya kuwa na mpango wa kando.

"Hapana.. Nipo kwenye ndoa yenye furaha na mke mmoja," Kabu alijivu mfuasi wa Instagram aliyehoji ikiwa ana mpango wa kando.

Mfanyibiashara huyo mashuhuri alipuuzilia mbali madai ya kutengana na mkewe na kusisitiza kwamba hawezi kumcheza mshirika huyo wake katika biashara. Pia alikana madai ya kuwa na mke mwingine.

Kabu hata hivyo alikiri kuwa na binti mkubwa mwenye umri wa miaka 24 ambaye alipata kabla ya kufunga ndoa na Sarah. Aliweka wazi kwamba mkewe anafahamu kuhusu binti huyo wake na hajawahi kumficha.

"Hapo kwa kuficha hapana, lakini yupo" Kabu alijibu shabiki aliyeuliza kuhusu uwezekano wake kuwa na binti mwenye umri wa miaka 24.

Simon na Sarah wamekuwa kwa ndoa kwa zaidi ya mwongo mmoja na tayari wamebarikiwa na watoto wawili pamoja, binti na mvulana.