"Nilipovunja sijengi!" Hatimaye Kajala amjibu Harmonize baada ya majaribio mengi ya kuomba msamaha

Muhtasari

•Hatimaye Kajala amejitokeza kumjibu mwanamuziki huyo ambaye walichumbiana naye kwa kipindi kifupi kwa njia ya mafumbo.

• Harmonize alikiri kwamba amekuwa akipitia kipindi kigumu tangu alipokosana na mwigizaji huyo mwaka jana na hadi kufikia hatua ya kuathirika kisaikolojia.

Harmonize na Kajala Masanja
Harmonize na Kajala Masanja
Image: HISANI

Siku za hivi majuzi mwanamuziki Rajab Abdul Kahali almaarufu kama Harmonize amekuwa akitia juhudi kubwa katika kumshawishi mpenzi wake wa zamani Fridah Kajala Masanja amrudie.

Katika juhudi hizo, Harmonize ambaye pia hujitambulisha kama Konde Boy ama Jeshi amemwandikia mwigizaji huyo jumbe kochokocho za kuomba msamaha kupitia mitandao ya kijamii na hata kuweka bango katika eneo la Kinondoni.

Hivi majuzi Harmonize alikiri kwamba amekuwa akipitia kipindi kigumu tangu alipokosana na mwigizaji huyo mwaka jana na hadi kufikia hatua ya kuathirika kisaikolojia.

"Nimekuwa sawa, nimekuwa nikitengeneza muziki lakini kuna wakati nilisema sasa imezidi. Mimi sina raha. Mimi ni Harmonize, naweza kutumia umaarufu wangu kupata mwanamke mrembo zaidi kumliko, nimejaribu na kila mtu anajua. Lakini ilifika wakati nikasema namtaka yeye tena. Nataka kila mtu ajue hali ambayo nimekuwa nikipitia. Imekuwa mbaya, siku tatu sikutoka nje, nilikuwa nakunywa dawa tu. Imekuwa tatizo kwangu. Ni kitu ambacho nahisi ndani yangu," Harmonize alisema.

Hatimaye Kajala amejitokeza kumjibu mwanamuziki huyo ambaye walichumbiana naye kwa kipindi kifupi kwa njia ya mafumbo.

Katika kile kilichoonekana kuwa ni ujumbe wa moja kwa moja kwa Harmonize, mwigizaji huyo alijirekodi akiwa ndani ya gari yake huku akiimba wimbo wa Rayvanny na Zuchu 'I miss you'. (Nakupeza) na kuweka video hiyo kwenye Instastori zake.

Kajala alichagua kupakia  kipande cha wimbo huo kinachosema, "Sipendi Tuchukiane,Japo Najua Mungu Amenilinda Na Mengi.Na sisemi Turudiane,Hilo Tambua Mie Nilipovunja,Sijengi Na Niliko Salama"

Huenda hiyo ni njia ya malkia huyo kumjibu Harmonize baada yake kujaribu kupata usikivu wake katika wiki mbili zilizopita.