Seneta Mwaura amsherehekea mwanaume aliyekubali kulea mtoto albino aliyeitwa jina lake, aahidi kufadhili elimu ya mkewe

Muhtasari

• Mwaura alitembeleafamilia ya mtoto albino aliyeitwa jina lake na kuahidi kumshughulikia kwa mahitaji yote na pia kufadhili elimu ya mamake mtoto huyo.

Seneta mwaura akiwa na familia na Ngure Gitonga na Whitney Nyamusi nyumbani kwao Ruiru
Seneta mwaura akiwa na familia na Ngure Gitonga na Whitney Nyamusi nyumbani kwao Ruiru
Image: Facebook

Seneta mteule Isaac Mwaura ambaye ni mlemavu wa Ngozi amehanikiza nyoyo za wengi baada ya kutembelea familia ambayo ilifanikiwa kupata mtoto mwenye ulemavu wa Ngozi na kumpa jina la Seneta huyo.

Mwaura ambaye ni mtetezi wa haki za watu wenye ulemavu wa Ngozi wiki chache zilizopita alielezea kwa maskitiko makubwa jinsi ambavyo babake aliitoroka familia yake baada ya kugundua kwamba Mwaura ni zeruzeru.

Akizungumza baada ya kukutana na familia hiyo ya Wilfred Ngure na Whitney Nyamusi wanaoishi eneo bunge la Ruiru, Mwaura alimpongeza Ngure kwa kutotoroka kama ambavyo babake yake alifanya miaka kadhaa nyuma alipozaliwa.

“Nimefurahiya sana kupata mtoto wa kiume aliyeitwa jina langu na Wilfred Ngure Gitonga na Whitney Nyamusi, wanandoa wachanga wanaoishi katika spinner, Ruiru. Nilishangaa sana Gitonga alipokuja kuniona kwenye mkutano ambao nilikuwa nikihudhuria karibu na anapoishi. Aliniambia kwamba alikuwa akinifuata kwa muda mrefu, na kwamba hadithi yangu ilikuwa imemtia moyo sana. Alipooa, mtoto wao wa kwanza wa kiume alikuwa na Ualbino, na aliamua kutotoroka kama baba yangu alivyofanya. Hapo ndipo walipoamua kumpa mtoto wao jina langu,” aliandika Mwaura kwenye Facebook yake.

Seneta Mwaura anayelenga kiti cha ubunge wa Ruiru aliahidi kuifadhili elimu ya chuo anuwai ya mwanamke huyo Whitney Nyamusi, elimu itakayochukua takribani miezi 7 na pia kushughulikia mahitaji maalum ya mtoto Isaac Mwaura Leon Junior.

“Tutamfadhili mama Whitney Nyamusi kwa kumpa kozi ya diploma ya urembo inayofadhiliwa kikamilifu kwa miezi 7 katika chuo cha Beauty Point. Zaidi ya hayo, ofisi yangu itawezesha mafuta ya kuzuia jua bila malipo, vifaa vya kujikinga na msaada mwingine wowote kwa mtoto na familia yake,” Seneta Mwaura alitoa ahadi.