"Nirudie tena" Harmonize amlilia Kajala huku akitundika picha yake kwenye chumba chake cha kulala

Muhtasari

•Harmonize ametoa ombi kwa Maulana arejeshe mahusiano yake na mwigizaji huyo huku akifungua moyo kwamba anampenda sana.

•Kajala hata hivyo amedokeza kwamba hayupo tayari kumrudia mwanamuziki huyo ambaye walitengana takriban mwaka mmoja uliopita.

Harmonize na Frida Kajala
Harmonize na Frida Kajala
Image: HISANI

Staa wa Bongo Rajab Abdul Kahali almaarufu kama Harmonize ameendelea kueleza hisia zake hadharani katika juhudi za kurejesha mahusiano yake na aliyekuwa mpenzi wake Fridah Kajala Masanja.

Mwazilishi huyo wa lebo ya Konde Gang alitambua mchora picha mmoja wa Bongo ambaye alichora picha ya Kajala na kuiagiza.

Baada ya kupata picha ile ya mpenzi huyo wake wa zamani, Harmonize aliendelea kuiweka hiyo kwenye ukuta wa chumba chake cha kulala.

"Wewe ndiye mtu pekee nitaona nikifungua macho yangu kila siku. Tafadhali rudi. Tabasamu kwa ajili yangu popote ulipo!!" Harmonize aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram huku akionyesha picha ya Kajala ikining'inia kwenye ukuta wa chumba chake.

Harmonize ametoa ombi kwa Maulana arejeshe mahusiano yake na mwigizaji huyo huku akifungua moyo kwamba anampenda sana.

"Nirudie tena!" Harmonize aliandika chini ya picha ya Kajala iliyoning'inia kwenye ukuta wake.

Kajala hata hivyo amedokeza kwamba hayupo tayari kumrudia mwanamuziki huyo ambaye walitengana takriban mwaka mmoja uliopita.

"Huwezi kuleta maisha yangu ya kitambo ili kunivunja, Hayo ndiyo Mungu alitumia kunijenga," Kajala alipakia kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Harmonize na Kajala walitengana Aprili mwaka jana baada ya kuchumbiana kwa miezi michache tu.