"Ameleta furaha kubwa katika familia" Kabi na Milly Wajesus wajivunia mtoto wao wa pili

Muhtasari

•Wakizungumza kupitia Youtube Channel yao, Kabi na Milly walifichua kwamba binti yao alizaliwa siku kadhaa zilizopita.

•Wazazi hao wa watoto wawili walifichua kwamba bado hawajakubaliana kuhusu jina la kumpatia mtoto wao mchanga.

Image: INSTAGRAM// KABI WAJESUS

Wanandoa mashuhuri Peter Kabi na Millicent Wambui wa 'The Wajesus Family' hatimaye wamemtambulisha hadharani mtoto wao wa pili.

Wakizungumza kupitia Youtube Channel yao, Kabi na Milly walifichua kwamba binti yao alizaliwa siku kadhaa zilizopita.

Wanandoa hao walisema walichelewesha hatua ya kumtambulisha binti yao kwa kuwa bado walikuwa wanajiandaa kwa hali yao mpya.

"Tumekuwa na mtoto kwa siku chache. Tulihisi tulihitaji kutulia mtoto kwanza aje nyumbani tumuelewe, nikumbuke kuosha mtoto, kumshika na kumyonyesha. Imechukua muda kutulia na mtoto," Milly alisema.

Wazazi hao wa watoto wawili walifichua kwamba bado hawajakubaliana kuhusu jina la kumpatia mtoto wao mchanga.

Kabi na Milly walisifia sana urembo wa binti yao na kufichua kwamba ameleta furaha kubwa na upendo mwingi katika familia yao.

"Yeye ni buheri wa afya. Yeye ni binti mfalme mrembo zaidi kuwahi kuwa. Ni mzuri sana, ameleta raha nyingi katika nyumba yetu. Taji anampenda sana. Sote tunapendana," Milly alisema.

Mtoto huyo ni wa pili kwa Milly na wa tatu kwa Kabi ambaye aliwahi kumtambulisha binti yake mwingine aliyezaliwa takriban miaka tisa iliyopita.