"Acha watoto wa kimaskini tutambe!" Harmonize ajibu madai ya kunua views

Muhtasari

•Harmonize amesema idadi kubwa ya watamaji ambao yeye na wasanii wake wamekuwa wakipata imetokana na talanta zao na bidii katika muziki.

•Konde Boy amesisitiza kwamba hatakubali kushushwa chini na madai hayo huku akisema amezoea kelele za mahasidi.

Image: INSTAGRAM// HARMONIZE

Mwanamuziki Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize ametupilia mbali madai kuwa amekuwa akinunua views za YouTube.

Akizungumza kupitia kurasa wake wa Instagram, Harmonize amesema idadi kubwa ya watamaji ambao yeye na wasanii wake wamekuwa wakipata imetokana na talanta zao na bidii katika muziki.

"Hawathamini bidii. Hawathamini talanta na jitihada kisa tu umetokea mtaani fikra zimezehekea wamekariri alitakiwa afanye jambo fulani, wewe hufanani kisa umetokea mtaani. Waambieni huu ndio wakati wetu. Acha watoto wakimasikini tutambe. Tulinyanyasika kwa muda sana kwa hiyo unataka Konde Boy ndo ana hela kuliko wasanii wote duniani," Harmonize aliandika.

Konde Boy amesisitiza kwamba hatakubali kushushwa chini na madai hayo huku akisema amezoea kelele za mahasidi. Amewashauri wanaoibua madai yale kukoma kuharibia Bongo jina.

"Acheni kuchafua habari zinazolibeba taifa aibu. Sawa na leo umshambulie Mwakinyo eti kapokonywa mkanda wakati heshima ulikuwa ukipata na wewe pia mtanzania!!" Alisema.

Bosi huyo wa Konde Music Worldwide ametangaza kwamba hatishiki na atakuwa anaachilia kibao kipya siku ya Alhamisi.