"Nimemalizana nawe kabisa!" Carrol Sonnie ampatia Mulamwah masharti makali ya msamaha

Muhtasari

•Muthoni amemwagiza mpenzi huyo wake wa zamani afunguke kuhusu ukweli wa yaliyotokea hadi kupelekea mahusiano  yao kugonga mwamba.

•Muthoni amemwambia Mulamwah kwamba hamtaki tena kwani tayari amemfuta kutoka moyoni mwake kabisa.

Image: INSTAGRAM// MULAMWAH

Mwigizaji Caroline Muthoni almaarufu Carrol Sonnie amesisitiza kwamba bado hajarudiana na baba ya bintiye, Mulamwah licha yao picha na video zao pamoja kusambaa mitandaoni.

Muthoni amewasihi wafuasi wake kutoanguka kwenye mtego wa picha hizo zao na kuweka wazi kuwa bado hajakubali kumsamehe mchekeshaji huyo.

"Msichezwe. Hakuna kitu kimesuluhishwa kati yangu na Mulamwah. Mwacheni awe mwanaume na achukue lawama yote," Muthoni alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Mwigizaji huyo amemtaka Mulamwah aombe msamaha, sio kwake tu bali pia kwa binti yao, familia na mashabiki wake kwa kile amesema, aliwapotosha.

Muthoni amemwagiza mpenzi huyo wake wa zamani afunguke kuhusu ukweli wa yaliyotokea hadi kupelekea mahusiano  yao kugonga mwamba.

"Masharti yangu ambayo hayawezi kupunguzwa ni; Omba msamaha kwa binti yako, Omba msamaha kwa familia yako, uwaombe msamaha mashabiki wako kwa kuwapotosha na kwa mara ya kwanza uongee ukweli," Muthoni alimwambia Mulamwah.

Haya yanajiri siku chache tu  ya Mulamwah kuibua madai mazito dhidi ya mamake huyo wa binti yake.

Miongoni mwa madai ambayo mchekeshaji alitoa dhidi ya Muthoni ni pamoja na kutokuwa mwaminifu katika kipindi cha mahusiano yao, kupachikwa ujauzito na jamaa mwingine, kutoa ujauzito na madai mengine ya kushangaza.

Kupitia ujumbe wa simu ambao alionyesha Instagram, Muthoni amemwambia Mulamwah kwamba hamtaki tena kwani tayari amemfuta kutoka moyoni mwake kabisa.

"Kwangu mimi nimemalizana nawe kabisa. Kama unamtaka kk kuwa maishani mwako unajua cha kufanya," Muthoni alimwambia mchekeshaji huyo.

Wawili hao walichumbiana kwa takriban miaka minne kabla ya mahusiano yao kugonga ukuta mwaka jana katika hali tatanishi.