Mwijaku awasuta WCB kutohudhuria msiba wa Maunda Zorro, Baba Levo amjibu vikali

Muhtasari

• Mwijaku aliwasuta WCB Wasafi kwa kutohudhuria msiba wa msanii Maunda Zorro wikendi iliyopita.

• Baba Levo alimjibu vikali mwijaku na kumtaka asitumie msiba kutafuta kiki kwa kuchafua jina la Wasafi.

Mwijaku, Diamond Platnumz
Mwijaku, Diamond Platnumz
Image: Instagram

Wikendi iliyopita, tasnia ya muziki nchini Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla iligubikwa ma majonzi baada ya kifo cha mwanamuziki Maunda Zorro aliyefariki kutokana na ajali ya barabarani.

Maunda Zorro ambaye ni dadake mwanamuziki mkongwe Banana Zorro alifariki baada ya gari lake kugongana dafrau la lori la mchanga na kuaga dunia papo hapo ambapo aliwaacha nyuma watoto wavulana watatu.

Msiba wake ulifanyika kwa taratibu za Kiislam ambapo watu wengi walihudhuria kumpa buriani mwanamama huyo. Lakini kubwa zaidi lililovuta nyuzi za wengi ni pale ambapo hakuna msanii hata mmoja kutoka lebo ya Wasafi aliyehudhuria msiba huo uliofanyika siku moja baada ya kifo chake.

Kama ilivyo kawaida yake, mtangazaji wa Clouds, Mwijaku alikuwa wa kwanza kupeleka mitandaoni kushtumu kitendo hicho cha Wasafi ambapo alisema hata kama walikuwa na tofauti awali, si vizuri kuendeleza uhasama huo kwani msiba ni kitu kinacho waleta watu wote pamoja na kuweka tofuti zao pembeni.

Wasafi nao si wachache wa hivyo kwani wana msemaji wao wa michambo, fundi manyumba Baba Levo ambaye aliamua kutokimya kabisa familia yake ya Wasafi ikisutwa na fundi wa michambo kutoka Clouds, Mwijaku.

Baba Levo alimkejeli Mwijaku kwa kusema kwamba anajaribu kutumia msiba wa Maunda Zorro kaam njia ya kuichafua brand ya Wasafi, jambo ambalo alisema limewashinda watu wengi kwa muda mrefu tu.

Katika kile kilichoonekana kama kumtupia vumbi machoni moja kwa moja Mwijaku, Baba Levo alisema si vizuri kutumia kiki kwenye msiba na kuonya kwamba wakitaka Wasafi nao waanze kutema makombora watayatema sana tena bila woga.