King Kaka afunga harusi ya siri na Nana Owiti?

Muhtasari

• King Kaka amedokeza kwamba tayari ameshafunga harusi na mkewe, Nana Owiti.

• Alisema kwamba anapenda mambo yake yakiwa siri.

Image: INSTAGRAM// KING KAKA

Rapa matata humu nchini, Kennedy Ombima almaarufu King Kaka amedokeza kwamba tayari ameshafunga ndoa na mke wake, Nana Owiti.

Akizungumza na wanablogu siku ya Jumanne, King Kaka alionyesha pete mkononi huku akisema kwamba harusi ilishafanyika kitambo.

Tayari ilikuwa ishapita zaidi ya miaka minne tangu amchumbie Nana huku wengi wakizidi kujikuna vichwa kuhusu mipango yake ya kufunga ndoa rasmi.

"Nikimchumbia nilikuwa na pete, sasa imetoka wapi? Mambo yangu nafanya chini ya maji,'' King Kaka alisema.

Japo kwa jinsi alivyojibu swali hilo, huenda ikawa alilenga kulipotezea tu, ila mashabiki na washikadau watalazimika kusubiri ili kufahamu kama ni kweli wawili hao tayari wameshafunga ndoa.

King Kaka alikuwa akiyazungumza hayo katika hafla rasmi ya kumzindua kama balozi wa rununu ya Itel huku akimshukuru mkewe kwa kumpa sapoti katika safari yake ya usanii na kimaisha kwa jumla.

Aidha, alisema kwamba Owiti amemsaidia pakubwa katika kujenga imani yake kwa kushiriki zaidi katika maombi. Alisema kwamba angependa sana mkewe awepo katika hafla hiyo ila alipatikana na majukumu mengine.

"Natamani angekuwa hapa, ila alikuwa na majukumu mengine kwa hiyo hangeweza kufika. Lakini ameniombea," Kaka aliongezea.

Kuhusu muziki, Kaka aliwataka wasanii kuzidi kutia bidii katika kazi zao kwani ndo njia pekee ya kuafikia mafanikio katika maisha na muziki wao.