Ndoto yangu ni kuwa kama Diamond Platnumz - Vincent Mboya

Muhtasari

• Vincent Mboya amesema kwamba anatamani kuwa kama Diamond Platnumz.

• Alisema kwamba angependa kuwa na umaarufu mkubwa kadri siku zinavyosonga.Image: HISANI

Mwanablogu matata nchini, Vincent Mboya amesema kwamba ndoto yake ni kuwa kama msanii Diamond Platnumz.

Akizungumza katika mahojiano ndani ya Obinna Tv, Mboya alisema kwamba anatamani kuwa na umaarufu mkubwa kama wa Simba, akisema kwamba hali hiyo itamsaidia kubadilisha maisha yake.

Aidha, alikiri kwamba anatamani mazingira ambapo mashabiki watakuwa wakiomba kupiga naye picha kila mahali anapoenda.

"...Yaani mimi natamani sana wakati ambapo kila mahali ninapoenda mashabiki wanaomba kupiga picha na mimi," Mboya alisema.

Mboya alisema kwamba kupitia umaarufu huo anaweza kupata nafasi kadhaa za ubalozi wa kampuni mbalimbali ambapo anaweza kuboresha maisha yake hata zaidi.

Kulingana naye, wasanii na mashabiki wa Tanzania wamefanikiwa kubadilisha kiki zao kuwa manufaa katika gemu la burudani huko Bongo na hivyo kuifanya sekta hiyo kuzidi kufana hata zaidi.

Ifahamike kwamba Wakenya wamekuwa wakimpiga vita Mboya, kwa kile walikisema kuwa anaingilia maisha binafsi ya wasanii. 

Ameshikilia kwamba ataendelea na kazi yake ya kuwakosoa wasanii wakati anapohisi kwamba wanaishi maisha ya uongo na kuwafumba macho mashabiki wao.