(VIDEO) MajiMaji na mamake walia kwikwi kwa kunyimwa tiketi ya ODM kuwania ubunge Seme

Muhtasari

• Maji Maji na mamake walia kwa kwikwi kwa kunyimwa tiketi ya ODM kuwania ubunge Seme

Mtangazaji na mwanamuziki Maji Maji wakikumbatiana na mamake kwa kilio
Mtangazaji na mwanamuziki Maji Maji wakikumbatiana na mamake kwa kilio
Image: Screenshots, video

Video ya mtangazaji na mwanamuziki wa kitambo Maji Maji wakilia katika kumbato na mama yake imezua gumzo pevu katika mitandao ya kijamii.

Inasemekana mtangazaji huyo ambaye mapema mwaka huu alitangaza kuwania ubunge wa Seme alidhulumiwa na chama cha ODM baada ya chama hicho kukataa kuandaa kura ya mchujo katika eneo hilo na badala yake kumkabidhi mbunge wa sasa James Nyikal tiketi ya kutetea kiti hicho.

Katika video hiyo yenye hisia kali, wawili hao wanasikika wakizungumza kwa lugha ya Dholuo ambapo inakisiwa mamake anamliwaza mwanawe kwa kunyimwa nafasi ya kugombea tiketi ya chama licha ya kuwa mwanachama wa muda mrefu wa chama hicho chenye umaarufu kuntu katika eneo pana la Luo Nyanza.

Maji Maji ni mtangazaji wa muda mrefu katika kituo kimoja cha redio humu nchini na pia alikuwa mwanamuziki miaka ya 2000 ambapo alishirikiana na mwenzake na kutoa kibao maarufu kwa jina ‘Unbwogable’

Kibao hicho kilijizolea umaarufu mkubwa enzi hizo mpaka kikawa ndicho kinatumika katika kampeni za uchaguzi mkuu wa 2002 na muungano wa NARC ambao ulikuwa ni mkusanyiko wa vyama kadhaa vilivyokuwa na dhamira la kuumaliza utawala wa hayati rais Daniel Moi ambaye alikuwa ameongoza kwa miaka 24.