"Acha kuhusisha kifo cha Kanumba na kudorora kwa viwango vya Bongo Movie" - Gabo Zigamba

Muhtasari

• Ni wakati sasa kifo cha Steven Kanumba kiache kuhusishwa na kudorora kwa viwango wa filamu za bongo.

• Gabo Zigamba alisema kufilisishwa kwa kampuni ya kusambaza filamu ndicho chanzo cha viwango duni vya filamu.

Salim Ahmed aka Gabo Zigamba na Steven Kanumba
Salim Ahmed aka Gabo Zigamba na Steven Kanumba
Image: Instagram, Twitter

Tangu mwaka 2012 wakati muigizaji nguli wa filamu za bongo Steven Kanumba kuiaga dunia, pamekuwa na minong’ono mingi tu huku baadhi wakisema tasnia ya filamu nchini Tanzania imezidi kuporomoka tangu kifo chake.

Pamekuwa na waigizaji wengi tena wazuri tu ila wengi wao wameshindwa kuyavalia vilivyo mawanda aliyoacha Kanumba, kwani ni kama yanawapwerepweta tu.

Baadhi ya wasanii sasa wamejitokeza kueleza wazi na kujitetea kutokana na kauli kwamba wengi wao hawaigizi kuelimisha bali wanaigiza tu kuchekesha mradi pesa.

Muigizaji nguli Salim Ahmed almaarufu kwa jina la kuigiza kama Gabo Zigamba amekuwa wa hivi karibuni kuliweka kwenye mizani ya maneno suala hilo kwamba tasnia ya filamu ya bongo ilikufa na kumfuata muasisi wake Kanumba.

Kulingana na Gabo Zigamba, viwango vya filamu za bongo vimeporomoka kwa kiasi kikubwa kutokana na kile alikitaja kwamba wasanii wengi wa kuigiza hawaamini tena katika kusambaza filamu zao kupitia kampuni ya ‘Steps Entertainment,’ kampuni ambayo ilivuma sana katika kusambaza filamu hizo kote Afrika kwa wapenzi wa Kiswahili.

“Kwa kuwa Distributors hawa ndio walikuwa wanajua wanataka nini, basi wao ndio walikuwa wanaongea na watayarishaji wa Filamu (Producers) kwamba watengeneze filamu za aina gani, hivyo walithibiti ubora wa filamu. Maana yake ni kwamba filamu za zamani zilikuwa na mvuto kwa sababu Steps walikuwa wakichukua filamu bora tu, hivyo producers walihakikisha wanaandaa filamu bora ili zikubalike kwa wasambazaji hao.” Alielezea mdau.

Taarifa zilizopo ni kwamba kampuni hiyo ya usambazaji ilifikia mwisho baada ya kupatana na ghadhabu ya serikali iliyoifilisi kwa madai ya kula kwa mgongo wa maslahi ya watayarishaji na hivyo msambazaji maalumu wa filamu akakosekana ikawa ni soko huria kwamba kila mwenye kamera anaweza kutoa filamu yake na kuisambaza kivyake hata kama viwango ni duni.