Aliyekuwa mfanyikazi wa Citizen TV apatikana amefariki ndani ya nyumba yake

Muhtasari

•Mtoa habari ambaye aliwasiliana na Mpasho alifichua kuwa Moses alikuwa akipambana na msongo wa mawazo kwa muda.

•Maafisa wa polisi walifika kwa marehemu Jumamosi asubuhi na kubaini alifariki siku kadhaa zilizopita.

Marehemu Cliff Moses
Marehemu Cliff Moses
Image: INSTAGRAM// CLIFF MOSES CLYYF

Mfanyikazi wa zamani wa Royal Media Services anayetambulika kama Cliff Moses amefariki dunia.

Mwili wa Moses ulipatikana ndani ya nyumba yake Jumamosi asubuhi. Haijathibitishwa wakati ambapo alifariki ila ripoti za awali zimeashiria huenda alijitoa uhai.

Marehemu alifanya kazi ya uhariri wa video katika kampuni ya RMS tangu 2017 hadi mapema mwaka huu wakati alipojiuzulu.

Mtoa habari ambaye aliwasiliana na Mpasho alifichua kuwa Moses alikuwa akipambana na msongo wa mawazo kwa muda.

Alifichua kuwa Cliff aliwahi jaribu kujitoa uhai baada ya kujiuzulu kutoka kazini takriban miezi miwili iliyopita.

Mapema wiki hii mfanyikazi mwenzake wa zamani aligundua kuwa simu yake ilikuwa imezimwa na hapo shughuli za kumtafuta zikang'oa nanga.

Maafisa wa polisi walifika kwa marehemu Jumamosi asubuhi na kubaini alifariki siku kadhaa zilizopita.

Hakikisha kuwa unawajulia hali jamaa na marafiki wako mara kwa mara. Huenda wamekumbwa na msongo wa mawazo na wanashindwa namna ya kujieleza. Wataalamu wanashauri uombe usaidizi unapokumbwa na msongo wa mawazo. Unaweza kuwasiliana na Red Cross bila malipo kupitia nambari 1199 ili kupata usaidizi.

Mungu ailaze roho ya marehemu pema peponi.