Mtoto wa tatu? Diana Marua ajibu madai kuwa ni mjamzito

"Kama kuna mtoto anakuja, ni vizuri. Watoto ni baraka," Diana Marua

Muhtasari

•Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumamosi, mama huyo wa watoto wawili alisita kukiri wala kukana madai hayo.

•Pia aliweka wazi kwamba hana shaka kuwa mume wake Bahati ataendelea kuwajibikia familia yake licha ya kuwa amejitosa siasani.

Diana Marua

Siku za hivi majuzi kumekuwa na tetesi kwamba mwanavlogu Diana Marua, na ambaye ni mke wa mwanamuziki Bahati ni mjamzito.

Uvumi huo ulianza baada ya video ya mcheza densi maarufu David Moya akimsurprise jukwaani kusambaa mitandaoni. Katika video hiyo, tumbo la Diana lilionekana kutokeza kidogo na baadhi ya wanamitandao wakadhani amebeba ujauzito.

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumamosi, mama huyo wa watoto wawili alisita kukiri wala kukana madai hayo.

"Kama kuna mtoto anakuja, ni vizuri. Watoto ni baraka. Nikiongeza baraka nyingine kwa familia, atakuja na sahani yake na nadhani hiyo ni baraka bora zaidi naweza patia mheshimiwa (Bahati)," Diana alisema.

Mwanavlogu huyo pia aliweka wazi kwamba hana shaka kuwa mume wake Bahati ataendelea kuwajibikia familia yake licha ya kuwa amejitosa kwenye ulingo wa siasa.

Diana alisema mumewe anajua kusawazisha kati ya kazi zake na familia na akasisitiza kwamba haoni kama siasa zitambadilisha.

"Yeye ndiye kielelezo bora cha mtu anayejua kusawazisha kila kitu. Sifikiri tofauti akibadilika kuwa mtu asiyewajibikia familia," Diana alisema.

Diana na Bahati wamekuwa kwenye ndoa kwa takriban miaka sita na tayari wamebarikiwa na watoto wawili pamoja.