Embarambamba amepigwa marufuku katika hafla za kiserikali

Muhtasari

•Msanii huyo kutoka Kisii alifichua kuwa amewekewa marufuku kutumbuiza katika shughuli za serikali.

Image: INSTAGRAM// EMBARAMBAMBA

Mwimbaji mwenye utata kutoka Kisii Chris Mosioma almaarufu Embarambamba ametoa wimbo wa kumwomboleza Rais Mwai Kibaki.

Mwimbaji huyo wa nyimbo za injili anayefahamika kwa mbwembwe zake aliambia Word Is kwamba alichagua kusherehekea rais wa tatu wa Kenya kwa wimbo kwa vile hakupata nafasi ya kutumbuiza alipokuwa hai.

Msanii huyo alifichua kuwa ingawa angependa kutumbuiza katika mazishi ya Kibaki, amewekewa marufuku kutumbuiza katika shughuli za serikali.

"Mara ya mwisho Uhuru alipokuja Kisii, niliambiwa nipunguze drama zangu kwani waliogopa ningezua mvutano," alisema.

"Mimi ni mtu poa tu na najua kujiendesha, nikipata nafasi nitakuwa poa sana, nipo Kisii na siwezi hata kuenda kutazama mwili wa Rais wetu Bungeni," alisema.

Video ya wimbo aliomtungia Kibaki inasambaa kwenye mitandao ya kijamii..

Katika video hiyo, Embarambamba amekaa kwenye shamba la mahindi akiwa amevalia suti nyekundu iliyochanika.

Kisha anainuka na kuanza kutembea huku na huko akiuliza, "Kifo umechukua Kibaki wapi ?”

Kwa mtindo wake wa kawaida, Embarambamba kisha anajitupa kwenye dimbwi lenye matope kabla ya kupanda mti huku akiomboleza.

"Kibaki ohhh. Kibaki umeenda wapi? Umefuata Moi”

Embarambamba alisema atamkumbuka Rais Kibaki kwa kuwezesha elimu bila malipo na kuwapa Wakenya katiba mpya.

Embarambamba alisema anamfuata mamake aliyekuwa akimtumbuiza Rais Daniel Moi huko Kisii.

"Nina talanta nyingi na nimekuwa kwenye tasnia kwa miaka 11."

Katika mahojiano yaliyopita, Embarambamba alisema aliamua kufanya muziki wa injili tofauti kwa kuingiza tamthilia.

Alimshukuru mkewe kwa kusimama karibu naye, akisema yeye ndiye anayefua nguo zake zenye tope baada ya maonyesho.

(Utafsiri: Samuel Maina)