"Nimechoka!" Mwanadada anayedai kuwa baby mama wa Ibraah amtaka ahudumie mtoto wao

Muhtasari

•Mishepu amedai kuwa Ibraah amemwachia majukumu yote ya mtoto wao, jambo ambalo limekuwa changamoto kubwa kwake.

•Amemshtumu mwanamuziki huyo kwa kuwa na 'utoto' mwingi huku akidai kuwa amekuwa akiogopa kuitwa baba.

Image: HISANI

Mwanadada anayedai kuwa mzazi mwenza wa staa wa Bongo Ibrahim Nampunga almaarufu Ibraah amejitokeza kwa mara nyingine kulalamika dhidi ya msanii huyo.

Kim Mishepu alitumia ukurasa wake wa Tiktok kuzua madai kuwa Ibraaah amepuuza majukumu yake ya uzazi licha ya kuwa walikuwa wameshiriki kikao na kuwa na makubaliano.

Kipusa huyo amedai kuwa Ibraah amemwachia majukumu yote ya mtoto wao, jambo ambalo limekuwa changamoto kubwa kwake.

"Mtoto ni mdogo anahitaji matunzo. Mimi ni mwanamke ambaye anapambana. Kuna wakati sio kwamba inabidi nishughulikie mtoto tu, niko na wadogo wangu ambao wananitegemea. Anavyokuwa ameniachia mimi nipambane kwa kila kitu inanipa ugumu sana. Kuna vitu vyangu vingi nashindwa kuvifanya sababu niko mwenyewe," Mwanadada huyo alisema.

Mishepu amesema alipojitokeza kulalamika kwa mara ya kwanza takriban miezi minne iliyopita aliweza kushiriki kikao pamoja na Ibraah na mjomba wake na wakawa na maelewano.

Amesema baada ya kikao hicho mjomba wa Ibraah alikuwa anafanikisha ushirikiano katika malezi ila baadae akakatiza mawasiliano.

"Nilipoona hivo nikamtumia mwanasheria wangu. Mwanasheria wangu aliongea na meneja wa Ibraah, akaongea na Ibraah mwenyewe lakini vitu vikawa haviendi poa," Alisema.

Kipusa huyo amesema kwa muda mrefu uhusiano wake  na Ibraah haujawa mzuri na ndio maana mjomba wake alikuwa daraja kati yao wawili.

Amemshtumu mwanamuziki huyo kwa kuwa na 'utoto' mwingi huku akidai kuwa amekuwa akiogopa kuitwa baba.

"Labda ana utoto. Nimemzidi umri kwa mwaka mmoja. Nimezaliwa 97 yeye amezaliwa 98. Kitendo cha kuitwa baba amekuwa akikiogopa sana. Drama ni nyingi. Ibraah hamhudumii mtoto. Amekuwa mtu mgumu. Hata hivyo ananiheshimu sana," Mishepu alisema.

Mishepu amesema kuwa yupo tayari kwa Ibraah kufanyia mtoto wake DNA ili kuthibitisha kuwa yeye ndiye baba mzazi.

"Ibraah naomba huduma za mtoto. Naomba tugawane sapoti. Nimechoka. Hata mimi ni binadamu napambana. Kuna wakati napata na kuna wakati nakosa. Nimechoka kwa haya mambo yenu," Amesema