'Tumepata pigo kubwa!' Akothee atoa heshima za mwisho kwa baba ya aliyekuwa mumewe Jared Otieno

Muhtasari

•Akothee amesema kifo cha Bw Otieno ni pigo kubwa kwao huku akimtakia marehemu mapumziko ya amani.

•Akothee aliandamana na mabinti wake wawili wa kwanza, Vesha na Rue Baby kuhudhuria mazishi hayo.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwanamuziki na mjasiriamali mashuhuri Esther Akoth almaarufu Akothee hivi leo yupo katika kaunti ya Migori kuhudhuria mazishi ya babu ya mabinti wake Vesha Okello, Rue Baby na Fancy Makadia.

Akothee amefichua baba mkwe wake Evans Otieno Maduma aliaga dunia siku kadhaa zilizopita na atakuwa anazikwa nyumbani kwake Kanga.

"Mapema leo nikielekea Kanga kutoa heshima za mwisho kwaa baba mkwe wangu. EVANS OTIENO MADUMA. Baba pekee mzazi kwa  mume wangu wa zamani Jared Okello Otieno na babu wa binti zangu," Akothee aliandika chini ya picha zake akiwa safarini kuelekea Migori.

Mama huyo wa watoto watano aliandamana na mabinti wake wawili wa kwanza, Vesha na Rue Baby kuhudhuria mazishi hayo. Amefichua kuwa Fancy Makadia hakuweza kujiunga nao kwa kuwa anafanya mtihani shuleni.

Akothee amesema kifo cha Bw Otieno ni pigo kubwa kwao huku akimtakia marehemu mapumziko ya amani.

Pamoja nami ni mabinti waJared Rue na Vesha . Fancy hakuweza kuwa nasi kwa kuwa ana mitihani. Tumepata pigo kubwa. RIP Baba. Kisha tutatembelea shule ya upili ya wavulana ya Kanga ambapo tuna kazi," Akothee ameandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Akothee na Jared walikuwa kwenye ndoa kwa takriban mwongo mmoja kabla yao kutengana mwaka wa 2005. Katika kipindi cha ndoa yao, wawili hao walibarikiwa na watoto watatu wa kike pamoja.

Baadae Akothee alijitosa kwenye mahusiano mengine yakiwemo na wazungu wawili ambao alipata nao watoto wawili wa kiume.

Kwa sasa Jared yupo kwenye ndoa nyingine ilhali Akothee anachumbiana na Nelly Oaks.