Diamond Platnumz kununua ndege mwaka huu? - Baba Levo adokeza

Alidokeza kuwa Diamond atakuwa mmiliki wa ndege kabla ya mwezi Oktoba.

Muhtasari

•"Nasema hivi! Ikifika mwezi wa kumi kama Diamond hajanunua ndege niuawe," Baba Levo amesema.

•Ingawa Diamond bado hajafanikiwa kununua ndege yake binafsi, mara nyingi ametumia ndege binafsi kufanya ziara zake za muziki.

Image: INSTAGRAM// DIAMOND PLATNUMZ

Mwandani wa Diamond Platnumz, Baba Levo amedokeza kuwa bosi huyo wa Wasafi anakusudia kununua ndege yake binafsi.

Akizungumza kupitia ukurasa wake wa Instagram, Baba Levo alidokeza kuwa Diamond atakuwa mmiliki wa ndege kabla ya mwezi Oktoba.

"Nasema hivi! Ikifika mwezi wa kumi kama Diamond hajanunua ndege niuawe," Baba Levo aliandika.

Msanii huyo amesisitiza kuwa yupo tayari kwa adhabu ya kifo iwapo ubashiri wake hautakuja kutimia.

Kwa muda mrefu Levo amekuwa miongoni mwa watu wa karibu zaidi na Diamond. Ingawa sio kila kitu wasemacho wasanii hutokea kuwa kweli, hatuwezi kupuuzilia matamshi ya Levo kutokana na ukaribu wake na Naseeb.

Ingawa staa huyo wa Bongo bado hajafanikiwa kununua ndege yake binafsi, mara nyingi ametumia ndege binafsi kufanya ziara zake za muziki.

Diamond aaminika kuwa miongoni mwa wasanii maarufu na tajiri zaidi, sio tu katika ukanda wa Afrika Mashariki bali pia kote Afrika.

Mapema mwaka huu alishirikishwa katika Filamu 'Young, Famous & African ambayo iliwahusisha wasanii wengine maarufu katika bara Afrika.

Diamond anafahamika kumiliki mali nyingi yenye thamani kubwa ikiwemo magari ya kifahari, manyumba makubwa, viwanja, mapambo ya thamani na nyinginezo.

Miezi kadhaa iliyopita baba wa kambo wa Diamond, Uncle Shamte alifichua kuwa msanii huyo anamiliki nyumba na viwanja 67 katika sehemu mbalimbali za Tanzania.

"Naseeb ana nyumba nyingi. Nyumba kama 67 . Mimi binafsi nina miaka  mitano kwenye familia, sasa nasimamia nyumba ya 61. Hatujipi sifa kusimamia nyumba lakini tunapozungumza sasa hivi hivyo ndivyo uwezo wake ulivyo" Alisema Uncle Shamte.

Shamte aliweka wazi kuwa nyumba hizo ni za kupangisha wala sio za Diamond kukaa huku akibainisha kuwa mwanawe hashindane na yeyote kwa utajiri.

Diamond kwa kawaida huwa hafichi utajiri wake na mara nyingi ameonekana akijigamba kuhusu vitu vya thamani kubwa alivyonunua.