Nadia Mukami afunguka kuhusu suala la kubadili dini

Muhtasari

•Mwanamuziki huyo amefichua kuwa mumewe hajawahi kumpatia shinikizo lolote la kubadilisha dini yake.

•Ameweka wazi kuwa huwa wanaelewana vizuri na kufurahia penzi lao licha ya tofauti za kidini zilizopo kati yao.

Image: INSTAGRAM// NADIA MUKAMI

Mwanamuziki Nadia Mukami ameweka wazi kuwa tofauti ya dini kati yake na Arrow Bwoy sio tatizo kwenye mahusiano yao.

Nadia amefichua kuwa mumewe hajawahi kumpatia shinikizo lolote la kubadilisha dini yake. Arrow Bwoy ni mfuasi wa dini la Kiislamu ilhali Nadia ni Mkristo.

 "Hajawahi kunipa pressure. Dini ni suala nyeti sana kwangu. Kuna vitu ambavyo sipendi kuzungumzia; serikali, dini, kikundi cha wachache ni mambo ambayo sipendi kuzungumzia kwa kuwa naweza kusema kitu kiumize mtu fulani na mashabiki ni aina tofauti," Nadia alisema akiwa kwenye mahojiano na Eve Mungai.

Malkia huyo wa muziki mwenye umri wa miaka 25 amesema kuwa kwa sasa upendo ndio dini yake na kipenzi chake.

Nadia ameweka wazi kuwa huwa wanaelewana vizuri na kufurahia penzi lao licha ya tofauti za kidini zilizopo kati yao.

"Huwa tunaombeana.Tuna furaha. Huwa tunaelewana. Kama vile wanandoa wengine huwa tunakosana kidogo. Kitu ninachopenda kutuhusu ni kuwa  tunaelewana  sana. Sisi ni marafiki, yeye ni bestie yangu. Tunafurahia hadi tukunje mgongo," Alisema Nadia.

Katika jamii ya Waafrika, ni kawaida kwa wanawake kubadilisha dini yao pindi wanapoolewa na mwanaume wa dini tofauti.

Mwanamuziki Tanasha Donna alipojitosa kwenye mahusiano na Diamond Platnumz alijiunga na dini ya staa huyo wa Bongo ya Kiislamu.

Wengi wamekuwa wakisubiri kuona ikiwa Nadia atapiga hatua kama hiyo baada ya mahusiano yake na Arrow Bwoy kuwa wazi.