Simpendi! Pritty Vishy azungumzia maisha baada ya kutengana na Stivo Simple Boy

Muhtasari

•Vishy amesema anaendelea vyema na tayari ameweza kusonga mbele na maisha yake baada ya kutengana na Simple Boy.

•Amesema kuna wanaume wengi  ambao wamekuwa wakimmezea mate na kumtongoza kupitia kurasa za mitandao ya kijamii.

Pritty Vishy, Stivo Simple Boy
Pritty Vishy, Stivo Simple Boy
Image: INSTAGRAM

Pritty Vishy ameweka wazi kuwa kwa sasa hakuna uhusiano wowote wa kimapenzi kati yake na aliyekuwa mpenzi wake Stivo Simple Boy.

Kipusa huyo amesema anaendelea vyema na tayari ameweza kusonga mbele na maisha yake baada ya kutengana na Simple Boy.

"Maisha yako sawa. Kila mtu ako na shughuli zake. Kuna mambo ambayo yamebadilika lakini sio mengi. Kila kitu kipo sawa," Vishy alisema katika mahojiano na Nicholas Kioko.

"Mimi  na Stivo hatuchumbiani. Hamtatuona pamoja. Ikitokea mtuone pamoja labda itakuwa kibiashara. Kwa sasa hamtaona tukichumbiana ama kutaniana"  Aliongeza.

Vishy alisema kwa sasa hana hisia zozote za kimapenzi kwa mpenzi huyo wake wa zamani. Hata hivyo aliweka wazi kuwa hana uhasama wowote dhidi yake.

"Simpendi Stivo Simple Boy. Simchukii lakini simpendi ile mapenzi," Alisema

Pia alidai tayari amefuta kumbukumbu zake na mwanamuziki huyo kutokea Kibra na kudai kuwa hampezi.

"Nilifuta kumbukumbu zote. Yeye ni historia kwangu. Sina kumbukumbu kwa sababu ni sharti nisonge mbele. Haina haja niweke kumbukumbu ambazo hazinisaidii ilhali akili yangu inafaa kuwa inahesabu pesa," Alisema.

Vishy alikuja kutambulika zaidi mapema mwaka huu kutokana na mahusiano yake na Stivo Simple Boy. Mahusiano yao yalifichuka hadharani baada ya video yao ambayo kipusa huyo alipakia kwenye TikTok kuvuma.

Wawili hao hata hivyo walitangazaa kutengana kwao mwezi jana huku Vishy akimshtumu Simple Boy kwa kuwa  na mahusiano na mwanadada mwingine.

Vishy ametangaza kuwa kwa sasa bado anatafuta mchumba mwingine. Amesema kuna wanaume wengi  ambao wamekuwa wakimmezea mate na kumtongoza kupitia kurasa za mitandao ya kijamii.

"Watu wanajua niko sokoni. Wanatuma meseji nyingi.  Hata watu wa kuuza mahindi wananitumia jumbe," Alisema.