Jovial awasuta wanamitandao waliomshtumu kwa kujaribu kumtongoza Rashid Abdalla

Muhtasari

•Jovial amewaagiza wanamitandao kukoma kumkashifu huku akieleza kuwa Rashid na mkewe ni wadosi wake.

•Lulu amemshukuru mwanamuziki huyo kwa kutumbuiza katika karamu yao na kumtakia mafanikio zaidi katika kazi yake.

Image: INSTAGRAM// LOULOU HASSAN

Mwanamuziki Jovial amewajibu wanamitandao ambao wamekuwa wakimkosoa kwa kusakata densi na mtangazaji Rashid Abdalla katika karamu iliyoandaliwa kusherehekea kuzaliwa kwake.

Jovial amewaagiza wanamitandao kukoma kumkashifu huku akieleza kuwa Rashid na mkewe ni wadosi wake.

Amesema wanawake wanaomkosoa wanatumia tukio la yeye kudensi na Rashid kufunguka matatizo yao ya kinyumbani.

Ninaona tu wanawake wakionyesha wasiwasi wao kwa kitendo kisicho cha hatia. Mumepata kisababu cha kufungua roho! Unaweza kuona wanakabiliana na mengi manyumbani kwao! Wanandoa hao ni wadosi wangu kwa wanaojua kipindi vizuri," Jovial alisema kupitia Instastori zake.

Malkia huyo wa muziki amewashauri wanawake kusuluhisha shida zilizo manyumbani kwao na kukoma kumtumia kama kisingizio.

"Mimi ni msanii na nilikuwa nafanya kazi yangu. Kwa habari yenu nililipwa pesa nzuri," Alisema.

Mtangazaji Lulu Hassan amethibitisha kauli ya Jovial kuwa yeye na mumewe ni wadosi wake. Amemshukuru mwanamuziki huyo kwa kutumbuiza katika karamu yao na kumtakia mafanikio zaidi katika kazi yake.

"Siwezi kushukuru vya kutosha Jovial. Umekusudiwa kwa makubwa, kando na kuwa wadosi wako sisi ni mashabiki wako. Endelea kupeperusha bendera  yako juu zaidi. Tunakupenda dada. Endelea kupaa zaidi," Lulu alisema.

Wikendi iliyopita Jovial alialikwa kutumbuiza katika karamu ya kusherehekea siku ya kuzaliwa ya Rashid.

Alipokuwa anatumbuiza alionekana akinengua kiuno na mtangazaji huyo wa Citizen TV kabla ya Lulu kuingilia kati na kumwondoa mumewe. 

Jovial amekuwa akipokea upinzani mkubwa kutokana na jambo hilo.