"Ninahisi salama nikiwa karibu naye" Willis Raburu abwagiwa sifa kemkem na mkewe

Muhtasari

•Namu amesema ameridhika na mume wake na mtoto wao ambaye alimtaja kuwa mzuri, mwenye upendo na mcheshi.

•Amesema yeye na mumewe wanafurahia hatua ya malezi na kufichua kuwa ujio wa mwanawe wao umemleta karibu zaidi na mumewe.

Image: INSTAGRAM// IVY NAMU

Mtangazaji wa Citizen TV Willis Raburu amepokea sifa kochokocho kutoka kwa mke wake Ivy Namu.

Namu ambaye ana asili ya Kenya na Uganda alikubali upendo, ukarimu, uaminifu na kujali kwa mumewe alipowashirikisha wafuasi wake katika kipindi cha maswali na majibu kwenye Instagram.

"Yeye ni mkarimu, ni mwaminifu, mtu anayemaanisha manenoyake. Najihisi salama nikiwa naye na sikuhitajika kuuliza hisia zake ama mipango yake na mimi kwa sababu ameweka jambo hilo wazi. Tena sihitajiki kubadilisha, kujificha ama kughushi chochote kunihusu (kizuri ama kibaya) nikiwa naye. Ninaweza kuwa asilimia 100 na hilo linanifanya huru na napenda hapa," Namu alisema kupitia Instastori zake.

Mama huyo wa mtoto mmoja alikuwa anamjibu shabiki aliyeuliza kuhusu sababu zake kumchagua Raburu kama mume wake.

Namu alisema ameridhika na mume wake na mtoto wao ambaye alimtaja kuwa mzuri, mwenye upendo na mcheshi.

"Yeye (Raburu) ni mtu wangu na tulitengeneza mtoto wa kupendeza zaidi, mwenye upendo na mcheshi. Moyo wangu umeridhika, Mungu alinijia," Alisema.

Katika kipindi hicho, Namu pia alilazimika kuzungumzia madai kuwa anatarajia mtoto mwingine hivi karibuni.

"Pamoja na mambo yote yanayozingira ujauzito, kwa kweli inafaa kuwa watu wanaohusika kutangaza habari kwa wakati wao wenyewe. Sijui, naona ni kukosa heshima kuuliza swali la kibinafsi kama hilo" Namu alisema.

Aidha alisema yeye na mumewe wanafurahia hatua ya malezi na kufichua kuwa ujio wa mwanawe wao umemleta karibu zaidi na mumewe.