Harmonize afichua kitu ambacho hawezi kudhubutu kufanya ndani ya gari la Kajala

Muhtasari

•Harmonize amesema kuwa anafurahia kuendesha magari aliyonunulia Kajala zaidi ya anavyohisi anapokuwa akiendesha magari yao.

•Mwanamuziki huyo alifichua kuwa hawezi kuvuta sigara ndani ya magari hayo kwa kuwa Kajala huwa hatumii sigara.

Image: INSTAGRAM// HARMONIZE

Ijumaa wiki iliyopita staa wa Bongo Harmonize alitangaza kuwasili kwa magari mawili aina ya Range Rover ambayo aliagiza kwa ajili ya aliyekuwa mpenzi wake Fridah Kajala Masanja.

Harmonize alionyesha magari hayo mawili kupitia mtandao wa Instagram na kumsihi mwigizaji huyo akubali kumsahe na warejeshe mahusiano yao.

"Nahisi kama kwamba  unahitaji kila nilicho nacho. Kila ninachomiliki, kwa asilimia fulani nahisi  unamiliki pia. Nakupenda sana na nakupenda sana. Naomba urudi nyumbani, tuishi maisha yetu kama zamani na Mwenyezi Mungu atatubariki tupate riziki zaidi ya tunayopata sasa hivi. Najuta sana. Pole kwako, pole kwa familia na pole kwa kila mtu. Tafadhali rudi, nakupeza sana," Harmonize alisema katika video aliyopakia Instagram.

Baada ya kutangaza kuwasili kwa magari hayo, Harmonize ameonekana akiyatumia kusafiri katika maeneo mbalimbali. Harmonize amepakia video kadhaa zikionyesha akiwa ndani ya magari hayo akienda na kutoka kufanya mazoezi katika Gym.

Bosi huyo wa Konde Music Worldwide amesema kuwa anafurahia kuendesha magari aliyonunulia Kajala zaidi ya anavyohisi anapokuwa akiendesha magari yao.

"Magari ya mpenzi wangu ni matamu zaidi kuliko yangu," Harmonize aliandika chini ya video moja.

Katika chapisho lingine, mwanamuziki huyo alifichua kuwa hawezi kuvuta sigara ndani ya magari hayo kwa kuwa Kajala huwa hatumii sigara.

"Sitadanganya. Inahisi vizuri kuendesha gari la mpenzi wangu lakini shida pekee niliyo nayo ni kuwa huwa havuti sigara. Kwa hivyo siwezi kuvuta sigara ndani ya gari lake," Alisema

Mashabiki wameendelea kutoa hisia tofauti kuhusiana na mambo makubwa ambayo Harmonize amekuwa akifanya katika juhudi za kurejesha mahusiano yake na Kajala.