Akothee awakejeli wanaume wasio waaminifu wanaodanganya wake zao kuwa wamekwama barabarani

Muhtasari

•Akothee amesema wanaume wasio waaminifu ambao wamezoea kudanganya wake zao kuwa wamekwama barabarani wapo taabani kwa kuwa Express Way imetatua shida za trafiki.

•Express Way ilijengwa katika juhudi za kukabiliana na msongamano wa magari ambao hushuhudiwa katika Mombasa Road na Waiyaki Way.

Akothee na mpenzi wake Nelly Oaks
Akothee na mpenzi wake Nelly Oaks
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Wakenya wameendelea kufurahia kutumia barabara ya Express Way tangu ifunguliwa kwa umma siku ya Jumamosi.

Katika kipindi cha takriban siku nne ambacho kimepita maelfu ya magari tayari yameweza kutumia barabara hiyo ambayo iligharimu Ksh72B.

Mwanamuziki Esther Akoth almaarufu Akothee ni miongoni mwa watu mashuhuri ambao wamefurahia jinsi barabara hiyo imeweza kupunguza msongamano wa magari.

Katika ukurasa wake wa Instagram, Akothee alipakia video inayoonyesha akisafiri kwa urahisi kwenye Express Way huku magari mengi yakiwa yamekwama kwenye barabara ya kawaida kando yake.

"Hawa watu mbona wasilipe kodi ili watumie Express Way. Hakuna msongamano hapa, watakuwa wanaambia wake zao ati kuna msongamano, hakuna trafiki Nairobi wanadanganya," Akothee alisikika akisema katika video hiyo.

Mama huyo watoto watano amesema wanaume wasio waaminifu ambao wamezoea kudanganya wake zao kuwa wamekwama barabarani wapo taabani kwa kuwa Express Way imetatua shida za trafiki.

"Wadanganyifu lazima watafute simulizi mpya. Simulizi ya trafiki imeisha.. Mtakoma, Hii ni Nairobi," Amesema.

Ujenzi wa Express Way ambayo imeanza Westlands hadi eneo la Mlolongo ulikamilika wiki chache zilizopita.

Wakati akizindua mbio za Nairobi City Marathon mnamo Mei 8, Rais Uhuru Kenyatta alisema barabara hiyo iko tayari kutumika na kutangaza ingefunguliwa kwa umma Mei 15.

Barabara hiyo ilijengwa katika juhudi za kukabiliana na msongamano wa magari ambao hushuhudiwa katika Mombasa Road na Waiyaki Way.