Odi wa Murang'a na Exray wajibu madai ya kumtenga Maddox, wajitolea kumlipia Rehab

Muhtasari

•Exray na Odi wa Murang'a wamefichua kuwa Boondocks alikosa kumakinika na muziki na badala yake kujitosa kwenye maisha ya anasa.

•Wawili hao walisema wamekuwa wakijaribu sana kumsaidia mwenzao huyo ila juhudi zao zote zimekuwa zikiangulia patupu.

Kundi la Boondocks Gang: Maddox, Odi wa Murang'a , Exray
Kundi la Boondocks Gang: Maddox, Odi wa Murang'a , Exray
Image: HISANI

Wanamuziki wa Gengetone ExRay na Odi Wa Murang'a wamejitokeza kujibu madai kuwa walimtenga mwanabendi mwenzao Maddox kutoka kwa kundi lao la Boondocks Gang.

Wawili hao wamesema mwanamuziki huyo mwenzao alikumbwa na masuala utovu wa nidhamu na hatimaye akajitenga nao mwenyewe.

Exray na Odi wa Murang'a wamefichua kuwa Boondocks alikosa kumakinika na muziki na badala yake kujitosa kwenye maisha ya anasa.

"Si mara moja ambapo tumeenda studio sisi wawili pekee, sio eti tunawanga tumemkaza ama hatujampasha habari. Ni juu yeye anataka kufanya vitu zake kando na kikundi. Ile wakati tumetenga kufanya mradi kama kundi la Boondocks unapata yeye ako shughuli zingine akija anapata tulishafanya. Kwa kuwa yupo kwenye kundi na hatuwezi kumtenga unapata tumetengeza ngoma tukamuachia verse yake kwa kuwa hakuwa wakati huo na tulijaribu kumfikia akakosekana," Odi wa Murang'a alisema akiwa kwenye mahojiano na Presenter Ali.

Exray alifichua kuwa  siku za hapo awali walikuwa wanasaidiana sana na Maddox hadi katika utunzi wa nyimbo.

Pia alifichua kuwa kwa muda mrefu amekuwa akiishi nyumba moja mwanamuziki huyo mwenzake hadi alipoondoka bila kumueleza sababu.

"Tulikuwa tunakaa na yeye nyumba moja. Kuna wakati ulifika akaniambia anahama. Hivo tu. Alihama akaenda mahali fulani. Alikuwa na pesa za nyumba. Wasimamizi huwa wanamshughulikia. Tuliona ni bora yeye ahudumiwe kuliko sisi," Exray alisema.

Wawili hao walisema wamekuwa wakijaribu sana kumsaidia mwenzao huyo ila juhudi zao zote zimekuwa zikiangulia patupu.

"Nilijaribu kumuongelesha mimi binafsi,ikafika mahali nikaona ni kama hanisikilizi, ikabidi tumepanga mkutano sote watatu kama Boondocks tukamuongelesha mimi na Exray. Bado hakubadilisha. Ilibidi tumeingiza watu wengine wakubwa wenye busara. Tumejaribu kutafuta watu wengine mbalimbali lakini wapi," Alisema Odi Wa Murang'a.

Wasanii hao wawili wamesema wapo tayari kumsaidia Maddox huku wakipendekeza apelekwe kwenye kituo cha marekebisho.

"Tuko tayari kumlipia rehab.Tayari tumemwambia. Marafiki wake sasa ndio wataamua," Walisema.

Hivi majuzi Maddox aliibua madai kuwa alitengwa kutoka kikundi chao cha Boondocks ambacho kilivuma sana mwaka wa 2018 na 2019.

Maddox alisema baada ya janga la Corona kukumba dunia kila mmoja wao alienda njia tofauti na hakuna aliyejihusisha naye.

Exray na Odi wa Murang'a hata hivyo wamesisitiza kuwa kundi lao bado lipo na wanakusudia kutoa muziki zaidi  pamoja.