"Nipo kwenye mahusiano!" Fahyma afunguka suala la kurudiana na Rayvanny

Muhtasari

•Fayvanny amesema ni kawaida yake na Rayvanny kusherehekea siku ya kuzaliwa ya mtoto wao pamoja kila mwaka.

•Fahyma ameweka wazi kwamba yupo kwenye  mahusiano dhabiti na mwanaume ambaye hakutambulisha.

fayvanny
fayvanny

Baby mama wa Rayvanny, Fahyma almaarufu Fayvanny ameweka wazi kuwa hatua ya kusherehekea siku ya kuzaliwa ya mwanawe pamoja na mwanamuziki huyo pamoja haina maana kuwa wamerudiana.

Akizungumza na waandishi wa habari katika hafla ya uzinduzi wa EP ya Hamisa Mobetto, malkia huyo alisema ni kawaida yake na Rayvanny kusherehekea siku ya kuzaliwa ya mtoto wao pamoja kila mwaka.

"Ni kawaida. Kila mwaka  sisi husherehekea siku ya kuzaliwa ya mtoto wetu. Sidhani kama kuna tofauti yoyote," Fahyma alisema.

Mama huyo wa mtoto mmoja alilazimika kuzungumzia suala hilo baada ya video yake na Rayvanny wakisherehekea siku ya kuzaliwa kwa mtoto wao kuzua tetesi za kurudiana miongoni mwa wanamitandao.

Fahyma amesema kuwa baba huyo wa mtoto wake ndiye alipo kwenye nafasi bora ya kusema ikiwa wapo pamoja au la. 

Ingawa alisusia kujibu iwapo bado anachumbiana na Rayvanny, Fahyma aliweka wazi kwamba yupo kwenye  mahusiano dhabiti na mwanaume ambaye hakutambulisha.

"Nipo kwenye mahusiano. Tena mahusiano serious. Ikifika muda mtaelewa, lakini nipo kwenye mahusiano. Sijawahi kuwa sipo kwenye mahusiano," Alisema.

Mlimbwende huyo aliendelea kudokeza kuwa mahusiano yake ya sasa huenda yakaishia kwa ndoa .

Tetesi za kutamatika kwa mahusiano ya Fahyma na Rayvanny zilienea takriban miaka mitatu iliyopita. Wawili hao walibarikiwa na mtoto wa kiume pamoja walipokuwa kwenye mahusiano.

Baada ya kutengana na mama huyo wa mtoto wake Rayvanny alijitosa kwenye mahusiano na binti ya muigizaji Kajala Masanja, Paula Kajala.

Hali halisi ya mahusiano ya Rayvanny na Paula hata hivyo haijulikani ilivyo kwa sasa  kwani kumekuwa na tetesi nyingi zilizoyazingira.