Nandy afunguka suala la ujauzito na mipango ya ndoa yake na Billnass

Muhtasari

•Nandy alieleza waandishi wa habari kuwa tayari wahusika wote wanajua tarehe ambayo yeye na mpenzi wake watafunga pingu za maisha.

• Uvumi wa Nandy kuwa mjamzito ulianza kutanda siku za hivi majuzi huku mashabiki wakihoji mabadiliko katika mtindo wake wa mavazi.

Image: INSTAGRAM// NANDY OFFICIAL

Malkia wa muziki wa Bongo Nandy amefichua kuwa harusi yake na mpenziwe Bilnass itafanyika hivi karibuni.

Nandy alieleza waandishi wa habari kuwa tayari wahusika wote wanajua tarehe ambayo yeye na mpenzi wake watafunga pingu za maisha.

Aliweka wazi kuwa harusi yake na Bilnass  itafanyika hadharani na itaendeshwa kwa kufuata miongozo ya Ukristo.

"Tutafunga ndoa siku chache zijazo. Tarehe zinajulikana kwa watu wahusika. Sio kitu cha siri kwa sababu sisi ni Wakristo lazima tuingie kanisani. Itakuwa harusi ambayo ni siku nzima," Nandy alisema.

Mwezi uliopita staa huyo wa Bongo alivishwa pete ya uchumba na Bilnass ambaye wamekuwa naye kwenye mahusiano kwa muda mrefu.

Wawili hao tayari wamekamilisha mipango ya kabla ya ndoa huku Bilnass akipeleka mahari kwa wazazi wa mkewe takriban miezi mitatu iliyopita.

Nandy vilevile amezungumzia madai kuwa tayari ni mjamzito. Uvumi kuwa yeye na mumewe wanatarajia mtoto hivi karibuni ulianza kutanda siku za hivi majuzi huku mashabiki wakihoji mabadiliko katika mtindo wake wa mavazi.

"Kama mimi ni mjamzito sidhani kama nitaficha. Kama mimi ni mjamzito sidhani kama tumbo litajificha. Nina vitu vingi vya kufanya siwezi kujificha ndani kama mimi ni mjamzito. Mtaona tu," Nandy alisema .

Hata hivyo alisema kuwa ni ombi lake kubeba ujauzito na kuweka wazi kuwa atashukuru sana wakati atakapofanikiwa.