"Kamwili kamerudi!" Onyi azungumzia mafanikio ya kipindi chake cha rehab

Muhtasari

•Onyi ameweka wazi kuwa kwa sasa ameacha kutumia dawa za kulevya na hayuko tayari kuwa mraibu tena.

•Onyi alisema rehab ilimsaidia kupambana na uraibu wa sigara, bangi, miraa na pombe ambazo zote alikuwa anatumia hapo awali.

Mwigizaji William Okore almaarufu Onyi
Mwigizaji William Okore almaarufu Onyi
Image: SCREEN GRAB// TUKO EXTRA

Muigizaji William Okore almaarufu Onyi amesema ameshuhudia mabadiliko mengi baada ya kuwa katika rehab kwa miezi mitatu.

Onyi ameweka wazi kuwa kwa sasa ameacha kutumia dawa za kulevya na hayuko tayari kuwa mraibu tena.

"Nimefurahia sana kwa sababu mwili umerudi. Tabasamu yangu pia imerejea. Nimeambiwa mpaka mashavu yameanza kuonekana. Nashukuru Mungu kuwa sasa niko sawa," Onyi alisema katika mahojiano na Eve Mungai.

Muigizaji huyo wa zamani wa Real Househelps of Kawangware alisema uraibu wake ulichangiwa na hali ya kutokuwa na kazi.

Alisema mashabiki wengi walipendekeza apelekwe katika kituo cha marekebisho baada yake kujitokeza kusimulia masaibu yaliyomkumba.

"Wataalamu walitambua mimi niko poa ni ukosefu wa kazi tu unanisumbua. Hapo ndio nikapelekwa rehab. Mimi  ndio nilikubali. Sikulazimishwa," Alisema

Onyi alisema rehab ilimsaidia kupambana na uraibu wa sigara, bangi, miraa na pombe ambazo zote alikuwa anatumia hapo awali.

"Raundi hii tumetalikiana nazo. Ndio maana ata natabasamu. Najivunia sana. Najaribu kuambia watu waepuke mihadarati," Alisema Onyi.

Muigizaji huyo ameahidi kuwa kioo cha jamii baada ya kufanikiwa kukamilisha kipindi chake cha marekebisho.

Pia ameahidi kuwajibika zaidi na kurejea kwenye kazi zake za usanii.

Onyi alijitokeza kueleza masaibu yake mwezi Machi mwaka huu. Alisema janga la Corona lilifanya afilisike kwani alipoteza kazi zake za usanii.

Alitoa ombi kwa watu kumpatia kazi ili aweze kukidhi mahitaji yake. Baadae alipelekwa kwenye kituo cha marekebisho ambao alikaa siku 90 akipambana na uraibu wa dawa za kulevya.