Mnaniangusha-Nyota Ndogo kwa marafiki wanaokula chakula kwenye hoteli yake na kukataa kulipa

Muhtasari
  • Hata hivyo, inaonekana kuna jambo linalomtatiza kuhusu marafiki wanaomtembelea pamoja na kuagiza chakula na kwenda bila kulipa
Image: INSTAGRAM// NYOTA NDOGO

Marafiki wanaweza kuwa wazuri mradi tu wanufaike na mwimbaji Nyota Ndogo anaonekana kuchoshwa na marafiki kama hao.

Msanii huyo hategemei tu usanii wake kwani amefungua hoteli yake sehemu za pwani ili kujikimu kimaisha.

Amekuwa akitangaza kazi yake na biashara yake kupitia mitandao yake ya kijamii.

Hata hivyo, inaonekana kuna jambo linalomtatiza kuhusu marafiki wanaomtembelea pamoja na kuagiza chakula na kwenda bila kulipa.

Alizungumza kwenye akaunti yake ya Instagram kwamba amekutana na marafiki wanaoagiza na kula chakula cha thamani ya Kshs. 4,000 na kwenda bila kulipa.

Kitu kinachomkera zaidi ni marafiki hao kumshukuru kwa chakula na kushindwa kuelewa kuwa biashara hiyo inahitaji pesa ili mambo yaendelee.

Kuna kodi ya kulipwa, wafanyikazi na hisa kwa biashara. Nyota Ndogo amewaita marafiki kama hao kuwa ni feki na walioazimia kuharibu biashara.

"Naomba msinichukulie vibaya tunao marafiki na mashabiki ,lakini kunao marafiki ambao wananikwaza sana,tunao marafiki ambao wanaulizia hoteli yangu wanakuja kama sita na wanaagiza chakula

Wakimaliza kula wanaingia kwenye gari na kuenda kisha wananishukuru,nina kodi ya kulipa watu wa kulipa kama nyinyi sio wanafiki mnasema mnakuja kunisupport,Kula bila kulipa sio kusaidiana mnaniangusha, na huo ni unafiki," Amesema Nyota.

Pia aliwashukuru kwa wale wamekuwa wakimsaidia kwa kazi yake.