Kinuthia asimulia jinsi huwa anachukuliwa kuwa mwanamke akiwa katika maeneo ya umma

Muhtasari

•Amesema amewahi kuzuiliwa kutumia vyoo vya wanaume mara kadhaa na kukaguliwa na walinzi wa kike baada ya kudhaniwa kuwa mwanamke.

•Alifichua kuwa mara nyingi yeye mwenyewe ndiye huenda dukani kununua mavazi ya kike ambayo huwa anatumia kutengeneza video zake.

Diana Marua na Kelvin Kinuthia
Diana Marua na Kelvin Kinuthia
Image: INSTAGRAM// DIANA MARUA

Mburudishaji wa TikTok Kelvin Kinuthia amefichua kuwa imetokea mara nyingi watu kudhani kuwa yeye ni mwanamke wanapomwona.

Kinuthia amefichua kuwa baadhi ya maeneo ambapo watu huchanganyikiwa kuhusu jinsia yake ni pamoja na katika vyoo vya umma, maduka makubwa na anapoagiza teksi.

Amesema amewahi kuzuiliwa kutumia vyoo vya wanaume mara kadhaa na hata kukaguliwa na walinzi wa kike baada ya kudhaniwa kuwa mwanamke.

"Katika maeneo ya kukaguliwa usalama kila ninapoombwa kuvuka kwenda upande mwingine wa wanawake huwa navuka kwa sababu siwezi kukaa hapo nibishane nao. Nikienda kwa wanawake mara nyingi huwa napata wananijua. Huwa naachwa tu nipite bila kukaguliwa," Kinuthia alieleza akiwa kwenye mazungumzo na Diana Marua.

Kinuthia hata hivyo aliweka wazi kuwa mara nyingi huwa anatumia vyoo vya wanaume na kukaguliwa na walinzi wa kiume.

Alifichua kuwa mara nyingi anapoagiza teksi madereva huonyesha shaka iwapo yeye ndiye aliyeagiza baada ya kumuona akiwa amevalia nguo za kike .

"Wakati mwingi huwa wanathibitisha kwa kuuliza kama ni Kelvin. Huwa nawaambia ni mimi. Lakini sasa niko sawa. Watu wamenizoea," Alisema.

Pia alifichua kuwa mara nyingi yeye mwenyewe ndiye huenda dukani kununua mavazi ya kike ambayo huwa anatumia kutengeneza video zake.

"Mimi huenda. Niko sawa. Si ni duka. Mimi huingia nachagua, naingia kwa chumba kubadilisha na nawauliza kama iko sawa. Mi huenda," Kinuthia alisema.

Muigizaji huyo hata hivyo alibainisha kuwa mara nyingi akiwa katika shughuli zake za kawaida huwa anavalia mavazi ya kiume.