Baha na mpenziwe wafichua mtoto wao alizaliwa kabla ya wakati

Muhtasari

•Baha na mpenzi wake Georgina Njenga wamefichua kuwa mtoto wao alilazimika kuwekwa kwenye incubator kwa siku kadhaa.

•Wawili hao wamefichua kuwa binti yao Astra Nyambura Kamau, alizaliwa Georgina akiwa na ujazito wa wiki 33 tu. 

Image: INSTAGRAM// TYLER MBAYA

Muigizaji Tyler Mbaya almaarufu Baha na mpenzi wake Georgina Njenga wamefichua kuwa mtoto wao alilazimika kuwekwa kwenye incubator kwa siku kadhaa.

Wawili hao walitangaza kuzaliwa kwa binti wao Mei 7, 2022 kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii. Hata hivyo hawakutoa maelezo mengi kuhusu mtoto wao kwa wakatai huo.

"Alikuja siku ya  kuadhimisha kuzaliwa kwangu. Tungependa kuwafahamisha nyie kuwa mtoto na mama yake wanafanya vizuri na wanatunzwa hapa hospitalini. Ni hadithi kubwa ya jinsi mambo yalivyotokea.Hatuwezi kusubiri kuwapeleka katika safari yote. Tunawapenda," Tyler alitangaza kupitia Instagram.

Kwenye akaunti ya Youtube ya Georgina Njenga, wapenzi hao wamepakia video ambayo walirekodi siku chache baada ya binti yao kuzaliwa.

Katika video hiyo, wawili hao wamefichua kuwa binti yao Astra Nyambura Kamau, alizaliwa Georgina akiwa na ujazito wa wiki 33 tu. 

"Kila kitu kilifanyika haraka. Tulipata mtoto wetu katika wiki ya 33. Lakini yeye ni msichana jasiri na mwenye afya," Georgina alisema.

Licha ya kuwaalijifungua mapema kwa takriban wiki saba, Georgina aliweka wazi kuwa mtoto wao alikuwa buheri wa afya na alikuwa anaweza kunyonya pamoja na kusongeza viungo vyake vya mwili.

Pia alifichua kuwa mtoto wao alilazimika kuwekwa ndani ya incubator kwa sababu hakuwa amefikia uzito wa kawaida wa mwili.

"Sababu kubwa ni suala la uzito wa mwili. Ni lazima wamuangalie. Ninachojua ni kuwa uzito wake unaweza kupungua sana na ndio maana ni lazima akae pale kwa siku kadhaa waone kuwa hapunguzi. Hata hivyo mtoto wetu ni mwenye afya na mwenye nguvu na ni ndiye mtoto mrembo zaidi," Georgina alisema.

Tyler na Georgina wamekuwa na Astra kwa takriban wiki nne sasa. Hata hivyo wawili hao bado hawajafichua sura ya binti huyo wao.