"Nina bahati sana kuwa baba yako," Harmonize amsherehekea bintiye kwa ujumbe maalum

Muhtasari

•Akisherehekea siku ya kuzaliwa ya bintiye, Harmonize alibainisha kuwa anajivunia sana kuwa baba yake Zuuh. 

•Shanteel alisema anajivunia sana Zuuh kuwa bintiye na kumhakikishi kujitolea maisha yake ili kumpa upendo usio na kikomo.

Image: INSTAGRAM// HARMONIZE

Binti wa pekee wa staa wa Bongo Harmonize, Zurekha Nasra almaarufu Zuuh Konde ametimiza miaka mitatu.

Zuuh ambaye ni mtoto wa Harmonize na Official Nana Shanteel aliadhimisha siku yake ya kuzaliwa Jumapili.

Akisherehekea siku ya kuzaliwa ya bintiye, Harmonize alibainisha kuwa anajivunia sana kuwa baba yake Zuuh. 

Harmonize alimtaja Zuuh kama rafiki wake wa dhati na kumhakikishia kuhusu upendo wake mkubwa kwake.

"Nakupenda sana rafiki yangu bora. Nina bahati sana kuwa baba yako. Kheri njema za kutimiza miaka mitatu kipenzi changu @zuuh_konde. Mungu akubariki," Harmonize alimwambia bintiye kupitia Instagram.

Bosi huyo wa Konde Music Worldwide aliambatanisha ujumbe wake na picha zinazoonyesha akiwa amembeba bintiye mikononi mwake.

Mamake Zuuh pia alimtakia kheri za siku ya kuzaliwa na kusema kuwa yeye  ni msukumo mkubwa kwake.

Shanteel alisema anajivunia sana Zuuh kuwa bintiye na kumhakikishi kujitolea maisha yake ili kumpa upendo usio na kikomo.

"Siku uliyozaliwa ilikuwa wakati mkubwa zaidi maishani mwangu!! Wakati unaenda haraka sana, juzi tu hungeweza kusimama na sasa napata kukuona ukikimbia! Nina bahati sana kwamba nilibarikiwa kupata binti mzuri kama wewe.. Wewe ni msukumo kwangu na natumai unahisi kuzungukwa na upendo na joto kwenye siku yako ya kuzaliwa. Nakuahidi kuwa nitajitolea maisha yangu yote kukupa upendo usio na kikomo. Heri ya kuzaliwa mpenzi wangu," Shanteel alimwandikia bintiye kupitia Instagram.

Desemba 2020 Harmonize alifichua kwamba alijitokeza kumfichua Zuuh na kukiri kuwa alimpata nje ya ndoa. Alisema alikuwa amemficha bintiye kwa zaidi ya miezi saba kwa kuhofia kuvunja ndoa yake.