Makena Kimathi afichua sababu zake za kususia kanisa

Muhtasari

•Makena alisema kuhudhuria kanisa au kutohudhuria hakuathiri uhusiano wake na Mungu ambao aliutaja kuwa wa kibinafsi.

•Makena alisema kanisa inafaa kutokuwa na ubaguzi na kuwakubali watu wote wakiwemo wapenzi wa jinsia moja.

Makena Njeri
Image: Studio

Mwanahabari wa zamani wa BBC Makena Njeri amefichua kuwa imepita zaidi ya mwaka mmoja tangu alipohudhuria ibada ya kanisa mara ya mwisho.

Akiwa kwenye mahojiano na Mpasho, Makena alisema kuhudhuria kanisa au kutohudhuria hakuathiri uhusiano wake na Mungu ambao aliutaja kuwa wa kibinafsi.

Mtetezi huyo wa haki za wapenzi wa jinsia moja alisema aliacha kuenda kanisa kutokana na unafiki mwingi unaoendelea pale siku hizi.

"Sidhani niko sawa kuenda kanisa kuona unafiki ambao huendelea mahali pale. Changamoto kubwa katika nchi hii hasa kwa jamii ya LGBTQ ni viongozi wa kidini. Unafiki ambao huendelea nyuma ya kuta zile tunazoita kanisa, sidhani unastahili kwangu. Niliacha kuenda kanisa lakini uhusiano wangu na Mungu ni wa kibinafsi," Makena alisema.

Makena alisema kanisa inafaa kutokuwa na ubaguzi na kuwakubali watu wote wakiwemo wapenzi wa jinsia moja.

"Sidhani kuna binadamu mdogo zaidi kuliko mwingine ambaye hafai kuingia kwa kanisa na aabudu na wengine kwa sababu ya jinsi walivyo. Nadhani kanisa inafaa kutenda kama inavyohubiri," Alisema.

Mwanaharakati huyo pia alifichua kuwa anatazamia kujitosa kwenye kazi za serikali katika siku zijazo.

Makena alisema analenga kutumia fursa hiyo kutengeneza mazingira bora kwa wapenzi wa jinsia moja.

"Katika siku zijazo tungependa kuketi katika nyadhifa za serikali ili kufanikisha mabadiliko. Sio kuketi tu kama rafiki,ni kuketi pale kama sehemu ya jamii ya LGBTQ  na mtu ambaye anaelewa changamoto zilizopo na nini kinafaa kufanyiwa ili kuleta mabadiliko," Alisema.

Makena pia aliweka wazi kwamba yeye huwa hajitambulishi na jinsia yoyote, iwe ya kiume ama ya kike.