Sitaki ufuate nyayo zangu!- Carol Muthoni amwambia binti yake na Mulamwah

Muhtasari

•Muigizaji huyo amesema nia yake ni kuona Keilah akienda mbali zaidi kuliko mahali ambapo yeye amefanikiwa kufika.

•Wiki iliyopita Mulamwah alipakia picha yake akiwa amemshika mtoto huyo mikononi na kumtambulisha kama bintiye.

Image: INSTAGRAM// CAROL MUTHONI

Aliyekuwa mpenzi wa Mulamwah, Carol Muthoni ameweka wazi kuwa hangependa bintiye mdogo afuate nyayo zake katika maisha.

Muigizaji huyo amesema nia yake ni kuona Keilah akienda mbali zaidi kuliko mahali ambapo yeye amefanikiwa kufika.

Muthoni alitoa matamshi hayo wakati akimsherehekea mtoto huyo wake wa takriban miezi tisa ambapo alimhakikishia kuhusu upendo wake mkubwa kwake.

"Binti yangu, sitaki ufuate nyayo zangu. Nataka uchukue njia iliyo karibu nami na uende mbali zaidi kuliko vile ningeweza kuota ingewezekana. Nakupenda mtoto K," Muthoni alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Siku za hivi majuzi Muthoni na mzazi mwenzake Mulamwah wamekuwa wakimuonyesha na kumsherehekea sana binti huyo wao kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii.

Hii ni licha ya madai ya hapo awali ya Mulamwah kuwa uhusiano mbaya kati yake na Muthoni ulikuwa unachangia ugumu wa malezi ya pamoja.

Wiki iliyopita mchekeshaji huyo alipakia picha yake akiwa amemshika mtoto huyo mikononi na kumtambulisha kama bintiye.

Mimi mdogo.. tumetulia @keilah_oyando," Mulamwah aliandika chini ya picha hiyo ambayo alipakia Instagram.

Wiki kadhaa zilizopita mchekeshaji huyo alidai kuwa miezi mitano ilikuwa imepita tangu mara yake ya mwisho kumuona binti yake.

Mulamwah ambaye pia ni muuguzi alidai hajawahi kupata nafasi ya kuwepo katika maisha ya binti yake.

"Nimeblockiwa kila mahali, wazazi wetu wamekasirikiana, mambo yameharibika. Familia yangu haijawahi kukutana na mtoto huyo tangu kuzaliwa kwake isipokuwa baba yangu ambaye alifunga safari kutoka Kitale kuja Nairobi. Tulikuwa tumepangia binti yangu karamu nyumbani, kila mtu alihudhuria lakini hakuja na K," Mulamwah alisema katika kipindi cha Maswali na Majibu (Q&A) kwenye Instagram.

Hata hivyo Muthoni alipkuwa ametembelea studio zetu mapema mwaka huu aliweka wazi kuwa hajamzuia mpenzi huyo wake wa zamani kumuona mtoto wao. Alitoa wito kwake kupiga hatua ya kutembea kwao ili kumuona.