Harmonize amteua Kajala kuwa meneja wake baada yao kurudiana

Muhtasari

•Kajala ataongoza timu ya mameneja wa Harmonize akishikilia wadhifa wa Mkurugenzi Mtendaji.

•Haya yanajiri wiki chache tu baada ya Harmonize kusema angependa sana muigizaji awe meneja wake.

Harmonize na Kajala
Harmonize na Kajala
Image: HISANI

Ni wazi kuwa Harmonize na muigizaji Fridah Kajala Masanja hatimaye wamekubali kuzika tofauti zao katika kaburi la sahau baada ya kukosana takriban mwaka mmoja uliopita.

Kajala sasa sio mpenzi tu bali pia ndiye meneja mpya wa mwanamuziki huyo. Pia ataongoza timu ya mameneja wa Harmonize akishikilia wadhifa wa Mkurugenzi Mtendaji.

Meneja wa usanii wa Harmonize Choppa TZ alitangaza habari za uteuzi wa Kajala huku akimkaribisha katika timu yao.

"Niruhusu nimkaribishe katika timu ya usimamizi mkurugenzi na meneja mpya Frida Kajala. Nimefurahi kufanya kazi na wewe shem," Choppa alitangaza kupitia Instagram.

Kajala sasa anaungana na Chopa, Mjerumani na Jose Wamipango katika timu ya usimamizi wa Harmonize na Konde Gang Music Worldwide.

Haya yanajiri wiki chache tu baada ya Harmonize kusema angependa sana mama huyo wa binti mmoja awe meneja wake.

Katika kipindi cha takriban miezi miwili ambacho kimepita Harmonize amekuwa akifanya majaribio mengi ya kumsihi Kajala akubali kumsamehea na kurudiana naye.

Huenda hatimaye bosi huyo wa Konde Music Worldwide amefanikiwa kumrejesha nyumbani muigizaji huyo ingawa bado hawajatangaza rasmi.

Siku ya Jumapili Kajala alijibu chapisho la Harmonize kwenye Instagram kwa mara ya kwanza tangu walipotengana.

Harmonize alichapisha ujumbe mrefu akimshukuru muigizaji huyo kwa kusimama naye katika hali zote licha ya mabaya aliyomtendea.

"Wakati Dunia Nzima inasema Haiwezekani Ulisimama Ukasema Inawezekana. Ulinipenda nami mbaya zaidi Ulikutana na Disappointment  ambayo iliwapa nguvu na ujasiri kila mtu aliye karibu yako kusema mimi sio binadamu wa kuwa hata karibu yako. Najua uliumia sana ...!!!! Bado hukunikatia tamaa. Wakati Mwingine binadamu huingia kwenye mahusiano ukiamini kwamba unaweza kumsahau yule uliyekuwa naye mwanzo bila kuwaza niini kiliwafanya muwe pamoja. Nilipitia hicho kipindi na picha zikamwagika mtandaoni na nikajiona nimemaliza wala sikujali maumivu yako. Bado ulikaa kimya, hakuna mahojiano licha ya kuahidiwa marundo ya pesa ambayo ungeweza kununua hata hivyo vigari wanavyoviona ni kitu cha maana sana,"  Harmonize aliandika chini ya picha ya Kajala ambayo alipakia Instagram Jumapil

Ni wazi kuwa ujumbe huo wa Harmonize ulimfikia mlengwa kwani chini yake Kajala alijibu kwa emoji zinazoashiria pongezi na upendo.

"🙏🏽🙏🏽🙏🏽❤️" Kajala alijibu.

Jibu la Kajala liliwasisimua mashabiki wengi wa Harmonize ambao walijumuika pale na kuacha jumbe nzuri za kheri.