Simiss ndoa yangu, nimepata takriban maombi 50 ya ndoa- Dadake Diamond afunguka

Muhtasari

•Esma alisema talaka sio  jambo geni kwake kwa kuwa hapo awali aliwahi kuwa katika ndoa zingine.

•Esma amefichua kuwa wanaume wengi wamekuwa wakiomba ndoa naye baada ya ndoa yake kusambaratika.

Diamond Platnumz, Esma Platnumz na Mama Dangote
Diamond Platnumz, Esma Platnumz na Mama Dangote
Image: HISANI

Dada ya Diamond, Esma Platnumz ameweka wazi kwamba hajawahi kuimiss ndoa yake na Maulid Yahya Msizwa.

Akiwa kwenye mahojiano na Global TV, Esma alisema talaka sio  jambo geni kwake kwa kuwa hapo awali aliwahi kuwa katika ndoa zingine.

Alisema tayari alikuwa na uzoefu wa kutengana kwa vile ndoa zake na awali na baba za watoto wake zilikuwa zimegonga ukuta pia.

"Sio ndoa yangu ya kwanza. Nilioana na Ba Tahiya, nikaja nikaoelewa na Ba Taraj. Kwa hiyo mimi sio mgeni wa ndoa," Esma alisema.

Mfanyibiashara huyo alitengana na Bw Msizwa takriban miaka miwili iliyopita baada ya kuwa katika ndoa kwa kipindi cha miezi michache tu.

Wawili hao walikuwa wamefunga pingu za maisha Julai 2020 katika harusi ya kufana iliyohudhuriwa na marafiki na wanafamilia wakiwemo Diamond na Zuchu.

Esma amefichua kuwa wanaume wengi wamekuwa wakiomba ndoa naye baada ya ndoa yake kusambaratika.

"Maombi yapo mengi sana. Kama ningekuwa nataka kuolewa naona sasa hivi ningekuwa kwenye ndoa kama 50. Wengine ambao hatukuwa tunachumbiana. Wengine ni marafiki tu," Alisema.

Mama huyo wa watoto wawili hata hivyo ameweka wazi kuwa amekuwa akiyapuuza maombi mengi ya ndoa ambayo amekuwa akipokea.

"Maombi mengi huwa yanaishia huko juu kwa juu kwa sababu sitakangi hayo mambo ya ndoa. Maombi yako mengi. Nashukuru Mungu labda nina nyota ya ndoa," Esma alisema.

Esma amesema kuwa kwa sasa anaangazia zaidi kwenye biashara yake ya nguo ila sio mahusiano.