Esma Platnumz afunguka kuhusu uhusiano wake na Mamake Diamond

Muhtasari

•Mfanyibiashara huyo alieleza kwamba alimchagua mamake Diamond kuwa rafiki yake mkubwa kwa kuwa nia yake kwake ni kweli.

•Alieleza kuwa huwa anahofia kuanzisha urafiki na watu wengine kwa kuwa wengi wao huja wakiwa na nia mbaya.

Image: INSTAGRAM// ESMA PLATNUMZ

Dadake Diamond, Esma Khan almaarufu Esma Platnumz amefichua kuwa hana marafiki wengi wa karibu.

Akiwa kwenye mahojiano na Global TV, Esma aliweka wazi kuwa Mama Dangote ndiye rafiki yake aliyekuwepo.

Mfanyibiashara huyo alieleza kwamba alimchagua mamake Diamond kuwa rafiki yake mkubwa kwa kuwa nia yake kwake ni kweli.

"Mimi nilichagua kukaa na mama yangu awe rafiki yangu kwa sababu nahisi yeye ndiye mtu ambaye ananisapoti sana kwenye kazi zangu. Hata nikianguka, yeye huwa ananisapoti sana," Alisema.

Esma alifichua kuwa mamake huwa anamsaidia sana hata katika kushugulikia wateja kwenye duka lake la nguo.

Alieleza kuwa huwa anahofia kuanzisha urafiki na watu wengine kwa kuwa wengi wao huja wakiwa na nia mbaya.

"Kuna rafiki anakuja kwako kwa sababu anataka kitu. Kuna mwingine anataka mkale bata. Kuna mwingine anakuja kukutongozea wanaume. Kuna marafiki wanakuja kwa umbea. Kila rafiki ana athari zake," Esma alisema.

Mfanyibiashara huyo pia alifichua kwamba huwa anatia bidii kubwa sana katika kazi yake kwa sababu anatamani sana kuwa tajiri kama kakake Diamond.

Alisema wivu wake kwa utajiri wa Diamond ndio unaomfanya ajitume zaidi katika biashara yake ya nguo.

"Mimi natamani niwe kama Naseeb. Sio eti niwe mwanamuziki lakini natamani yale maendeleo yake. Ili niwe kama yeye ni kujituma kwa bidii," Esma alisema.

Mama huyo wa watoto wawili vilevile aliweka wazi kuwa kamwe hawezi kujibweteka eti kwa kuwa kaka yake ni tajiri mkubwa.

Alisema hawezi kufikiria kutegemea utajiri wa Diamond maishani kwa kuwa ni jambo ambalo linaweza kumletea dharau.

"Unapomuona mwenzio tajiri nawe unatamani kuwa kama yeye. Kutamani kuwa kama yeye ni kufanya kazi kwa bidii. Sio kwa sababu eti ndugu yako tajiri eti ujibweteke, kwanza utadharaulika. Wafanyikazi wake na watu wa karibu pia watakudharau. Utafikia mahali ambapo ata mbwa wake watakudharau," Alisema.

Esma alisema kwamba huwa anapendelea kuwa katika duka lake la nguo kwa kuwa wateja wake wengi hupenda awahudumie mwenyewe.