Bado tuna matumaini-Anerlisa Muigai avunja kimya baada ya Keroche kufungwa tena

Muhtasari
  • Ikumbukwe kwamba kampuni hiyo ilifungwa tena mapema mwaka huu kutokana na masuala sawa
Anerlisa Muigai
Image: Anerlisa Muigai/INSTAGRAM

Mfanyabiashara mashuhuri Anerlisa Muigai hatimaye amevunja ukimya, saa chache baada ya habari kuenea kwamba kampuni ya  Keroche Breweries ilikuwa imefungwa tena.

Kupitia akaunti yake ya Instagram, mrembo huyo alikiri kuwa hizo zilikuwa nyakati za bahati mbaya sana kwa familia yake kwa ujumla, na kueleza zaidi kwamba wanamwamini Mungu kuwaokoa katika dhiki hizo.

"Walisema ikinyesha huwa yanamwagika ... kwa bahati mbaya ndivyo imekuwa ikitokea kwa upande wa familia yangu lakini nadhani nini, bado tuna matumaini kwa siku zijazo na bado tunamshukuru Mungu kwa kila kitu..." aliandika.

Chapisho la Anerlisa Muigai bila shaka ni la kweli kwa sababu wiki chache zilizopita, pia alikuwa na matatizo yake mwenyewe baada ya dalali fulani kujaribu kuvamia nyumba yake ya Nairobi kutokana na deni alilodaiwa ambalo lilikuwa Kshs. 3,399,148.45.

Kampuni ya Keroche Breweries ilifungwa siku ya Jumanne, na hii ilikuwa ni baada ya makubaliano ya jinsi itakavyolipa malimbikizo ya ushuru kukosa kuafikiwa.

Kulingana na ripoti, pia ilidaiwa kuwa kampuni hiyo ilikiuka makubaliano ya awali na KRA, ambapo walitakiwa kulipa malimbikizo ya ushuru hatua kwa hatua.

Hata hivyo hili ni jambo ambalo kampuni hiyo ilikanusha.

Ikumbukwe kwamba kampuni hiyo ilifungwa tena mapema mwaka huu kutokana na masuala sawa.

Hata hivyo makubaliano yaliafikiwa mwezi Machi ambapo kampuni hiyo ilipaswa kulipa KRA Kshs 957 milioni katika muda wa miezi 24 kuanzia Januari 2022.